Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kushirikiana na wananchi na wadau wengine katika kuimarisha ulinzi na usalama wa maisha na mali kwa kubuni na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kubaini na kuzuia uhalifu. Pia limeendelea na oparesheni, misako na kufanya uchunguzi wa matukio machache yaliyotokea na kufanyika na kufanikiwa kuwakamata wahalifu wa makosa mbalimbali.

Kwa kipindi cha mwezi Juni, 2026 kutokana na mikakati hiyo jumla ya watuhumiwa 239 wa uhalifu ikiwemo Mauaji, kujeruhi, kubaka, kupatikana na silaha bila kibali, kupatikana na dawa za kulevya na matukio ya wizi walikamatwa. Miongoni mwa watuhumiwa waliokamatwa na upelelezi wa kesi zao kukamilishwa walifikishwa Mahakamani.

Aidha, watuhumiwa watatu ambao ni Yella Mboya [27] mkazi wa Tunduma Mkoa wa Songwe, Furaha Mboya [25] mkazi wa Isongole na Elisa Mboma [43] mkazi wa Isongole wanashikiliwa kwa tuhuma za mauaji ya Bibi yao aitwaye Mary Mwasile [70] aliyekuwa mkazi wa Kijiji cha Isongole.

Tukio hilo lilitokea Juni 28, 2026 saa 4:30 asubuhi maeneo ya Isongole, Kijiji cha Isongole, Kata ya Santilya, Tarafa ya Isangati ambapo Mary Mwasile alikutwa ameuwawa ndani ya nyumba yake kwa kuchomwa kitu chenye ncha kali shingoni.

Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kupitia Kikosi maalum cha Askari wa kuzuia na kupambana na matukio ya mauaji lilianza ufuatiliaji wa tukio hilo na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao watatu. Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio ni imani za kishirikina.

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Askari Wanyamapori [TAWA] linawashikilia watuhumiwa watatu, Shughuli Halezya [50], Shabani Matulu [36] na Baraka Mwaluswaswa [26] wote wakazi wa Lualaje kwa tuhuma za kupatikana na Silaha aina ya Gobole bila kibali.

Watuhumiwa walikamatwa Juni 30, 2026 katika msako uliofanyika Kijiji cha Bitimanyanga, Kata ya Mafyeko, Tarafa ya Kipembawe, Wilayani Chunya. Watuhumiwa walikutwa wakiwa na Silaha moja aina ya Gobole, Bering 22, Goroli 13 zinazotumika kama risasi katika silaha hiyo, Fataki 15 na Kopo moja dogo la Baruti. Uchunguzi wa awali umebaini kuwa watuhumiwa ni wawindaji haramu.

Sambamba na hayo, kwa kipindi cha mwezi Juni, 2026 jumla ya watuhumiwa 9 walikamatwa wakiwa na dawa za kulevya aina ya bhangi kilo 94.44, watuhumiwa 2 walikamatwa wakiwa na pombe haramu ya moshi maarufu Gongo lita 41, watuhumiwa 5 walikamatwa wakiwa na bidhaa za magendo zenye thamani ya shilingi 6,523,000/=, bidhaa hizo ni Mafuta ya kula aina ya Nona lita 440, Sukari katoni 200, Vipodozi boksi 12 na Pombe kali zilizopigwa marufuku nchini katoni 59.

Katika kutekeleza mikakati ya kuzuia na kudhibiti ajali za barabarani Mkoa wa Mbeya, kwa kipindi cha mwezi Juni, 2026 jumla ya madereva 7 wamefungiwa leseni za udereva kutokana na kufanya makosa yanayojirudia, ikiwemo kusababisha ajali na kutenda makosa hatarishi ikiwemo mwendo kasi na kupita magari mengine kwenye maeneo hatarishi kama vile kwenye kona na milima maeneo ambayo siyo rahisi kuona magari yanayo kuja mbele.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kutoa shukrani kwa wananchi kwa kuendelea kutoa ushirikiano katika kubaini na kuzuia uhalifu. Pia linatoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili kuzuia na kutokomeza uhalifu. Aidha, linatoa wito kwa baadhi ya wananchi wanaoendelea kujihusisha na uhalifu kuacha mara moja kwani uhalifu haulipi.

Imetolewa na:
Kamanda wa Polisi,
Mkoa wa Mbeya.