Na. Mwandishi wetu – Zanzibar
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) inafungamanisha uchumi wake na Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 kupitia uwekezaji mkubwa uliofanywa ikiwemo kujengwa kwa miundombinu katika viwanja vya michezo vitakavyotumika wakati wa michuano hiyo.
Hayo yamelezwa leo Julai 02, 2026 na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Makatibu Wakuu ya Maandalizi ya Michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (AFCON 2027), Dkt. Jim Yonazi, walipotembelea na kukagua maandalizi kuelekea michuano hiyo Zanzibar na kuonesha kuridhishwa na hatua mbalimbali zilizofikiwa.
Dkt. Yonazi ameiongoza Kamati hiyo iliyotembelea viwanja vitakavyotumika wakati wa michuano hiyo ikiwemo cha Fumba unaojengwa Mkoa wa Mjini Magharibi, na Uwanja wa New Amaan Complex na kusema hatua mbalimbali za ukarabati zinaendelea ikiwemo upande wa miundombinu itakayotumika wakati wa michuano ili kuhakikisha inakidhi viwango vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kabla ya michuano kuanza.
Akiongelea maandalizi ya kuelekea michuano hiyo Dkt. Yonazi amesema, Serikali ya Tanzania imejipanga kikamilifu kwa kuweka mikakati thabiti inayojumuisha ujenzi na ukarabati wa viwanja vya michezo, uboreshaji wa miundombinu ya barabara, usalama, na utangazaji wa vivutio vya utalii kimataifa ili nchi inufaike kiuchumi na kuitumia michuano hiyo kama kichocheo cha uwekezaji katika soka la vijana na kuongeza hamasa ya michezo pamoja na kuongeza fursa za ajira, na kuimarisha diplomasia.
“Kamati imeendelea na uratibu kuelekea michuano ya AFCON 2027 ili kujiridhisha na maendeleo ya ujenzi na ukarabati wa viwanja vitakavyotumika katika michuano hiyo kwa kuzingatia umuhimu wake kwa Taifa letu hivyo tumewekeza nguvu nyingi kwani haya sio tu mashindano ya soka bali ni jukwaa kubwa la kuitangaza Tanzania na vivutio vyake kimataifa,” alisema Dkt. Yonazi
Aidha alisema kuwa, maandalizi yamehusisha maboresho makubwa ya eneo la kuchezea, viti, na taa ili kukidhi vigezo vya CAF. Pia, kamati ilikagua maendeleo ya mradi mkubwa wa ujenzi wa uwanja mpya wa kisasa wa Zanzibar Arena katika eneo la Fumba. Uwanja huo wa Fumba wenye uwezo wa kuchukua mashabiki wengi na unaojengwa kwa ubora hivyo kila sekta iendelee kujipanga ili kuhakikisha michuano hiyo inafanikiwa na kwa viwango vinavyotakiwa.
“Ukaguzi huo unadhihirisha utayari na dhamira ya Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha miundombinu muhimu ya michezo inakamilika kwa viwango vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), ili kufanikisha mashindano haya ya kihistoria yatakayoanza rasmi mwaka 2027,” alisisitiza Dkt. Yonazi.
Dkt. Yonazi ametoa wito kwa sekta binafsi kuchangamkia fursa za kiuchumi kupitia sekta ya utalii, huduma za malazi (hoteli), na utamaduni.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Bw. Salhina Mwita ameishukuru Kamati kwa kutembelea na kukagua maandalizi hayo huku akieleza mikakati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayofanya ukarabati wa viwanja mbalimbali vitakavyotumika kwa ajili ya mazoezi ya timu shiriki za michuano hiyo.
“Tumefarijika na ujio wa kamati na tunaahidi kuendeleza mashirikiano ili kuhakikisha mashindano yetu yanafanyika ipasavyo na kwa mafanikio makubwa,” alisema Bw. Mwita

