NA DENIS MLOWE IRINGA
MKUU wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta, ameutaka uongozi wa Manispaa ya Iringa kuhakikisha asilimia tano ya ongezeko la mikopo ya mapato ya ndani ya halmashauri inaelekezwa katika kuboresha mazingira ya biashara kwa wajasiriamali wadogo ili waweze kufanya shughuli zao katika maeneo rafiki na yenye tija.
Sitta alitoa kauli hiyo wakati wa hafla ya ugawaji wa mikopo ya zaidi ya shilingi milioni 400 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, ambapo alisema uamuzi wa Serikali kuongeza kiwango cha mikopo kutoka asilimia 10 hadi asilimia 15 unalenga kuimarisha mazingira ya biashara kwa wananchi.
Alisema changamoto kubwa inayowakabili wajasiriamali wengi ni ukosefu wa maeneo mazuri ya kufanyia biashara, hivyo aliutaka uongozi wa Manispaa kutumia sehemu ya fedha hizo kununua au kufidia maeneo yatakayowezesha wafanyabiashara wadogo kufanya kazi kwa urahisi.
“Maelekezo ya Serikali ni kuhakikisha ongezeko hili linaleta matokeo chanya kwa wajasiriamali kwa kuboresha mazingira yao ya biashara,” alisema Sitta.
Awali, Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo, alisema pamoja na Manispaa ya Iringa kutokuwa na mapato makubwa ikilinganishwa na halmashauri nyingine, imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kupitia mikopo hiyo.
Alimpongeza Mkurugenzi wa Manispaa kwa kusimamia vizuri fedha hizo na kuhakikisha zinawafikia walengwa, huku akieleza kuwa Bunge tayari limepitisha utaratibu wa kuongeza mikopo ya halmashauri kutoka asilimia 10 hadi asilimia 15 ya mapato ya ndani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Zaina Mlawa alisemq kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026 halmashauri imetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.2 kwa makundi mbalimbali.
Alisema katika hafla hiyo jumla ya zaidi ya shilingi milioni 400.2 zimetolewa kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu pamoja na vitendea kazi ikiwemo bajaji na pikipiki.
Naye afisa maendeleo ya jamii Manispaa ya Iringa Mwantumu Ndosi alisema vikundi 49 vilivyowasilisha maombi katika robo ya nne havikupata mikopo kutokana na kutokidhi vigezo vilivyowekwa.
Vikundi hivyo vinajumuisha 26 vya wanawake, 21 vya vijana na viwili vya watu wenye ulemavu, ambavyo kwa pamoja viliomba mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 782.
Akizungumza kwa niaba ya wanufaika, Joseph Sanga mmoja wa wawakilishi wa vikundi vilivyopokea mikopo hiyo aliishukuru Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na uongozi wa Manispaa ya Iringa na madiwani kwa kuwawezesha kupata mtaji utakaosaidia kukuza biashara zao na kuboresha maisha yao.