WAZIRI MKUU Dkt Mwigulu Nchemba amewabana Mameneja wa RUWASA na TANROADS mkoani Mara kwa kuwahoji maswali huku akiwaonya wasizoee matatizo ya wananchi na kuyaona ni mambo ya kawaida.
Akizungumza na wananchi waliofika kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika leo mchana (Alhamisi, Julai 02, 2026) kwenye viwanja vya Obwere, kata ya Shirati, wilayani Rorya, mkoani Mara, Waziri Mkuu alianza na Meneja wa RUWASA, Mhandisi Charles Pambe kwa kumhoji ni kwa nini wamekuwa na mgao wa maji katika mji wa Shirati uliopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Rorya.
Akijibu swali hilo, Mhandisi Pambe alisema walikuwa na changamoto ya miundombinu ya pampu na mabomba ya maji yenye urefu wa kilometa nne. Mahojiano yake yalikuwa kama ifuatavyo:
Waziri Mkuu: Pampu ni bei gani?
Mhandisi Pambe: Shilingi milioni 300 na kuna mabomba yameharibika ya km.4.
Waziri Mkuu: Shilingi milioni 300 ndiyo zinasababisha wananchi wakose maji? Wewe kwako ulikuwa na mgao wa maji?
Mhandisi Pambe: Hapana Mheshimiwa.
Waziri Mkuu: Ulishawahi kufika ziwani?
Mhandisi Pambe: Ndiyo Mheshimiwa Waziri Mkuu
Waziri Mkuu: Kwenda ziwani kwa miguu inachukua miaka mingapi?
Mhandisi Pambe: Ni masaa tu na wala haifiki siku moja.
Waziri Mkuu: Wananchi walioko mwendo wa masaa tu kwenda ziwani, inakuwaje wanapata mgao wa maji hapa Rorya, wakati wewe unaenda kazini kila siku? Mambo gani haya ya ajabu. Watendaji tusijisahau na kuzoea shida za wananchi.
Ndipo Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Mathew Kundo aliomba kipaza sauti na kumweleza Waziri Mkuu kwamba ameshawaelekeza wahusika watafute hiyo pampu ndani ya mwezi huu ili wananchi wasipate changamoto ya maji.
Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS wa mkoa huo, Mhandisi Musa Madirisha Kaswahili aliulizwa ni lini watatangaza tenda ya ujenzi wa barabara ya kutoka Shirati hadi Utegi yenye urefu wa km. 27 alisema watapitia upya mchakato wa awali na huenda wakawa tayari ifikapo Agosti, mwaka huu.
Alipoulizwa ni kwa nini inachukua muda mrefu hivyo, Mhandisi Kaswahili alijibu kwamba wanataka kupitia upya vigezo vya tenda kuviboresha. Alipoulizwa ni kwa nini inachukua muda mrefu wakati tenda ilishatolewa tayari na mkandarasi alishatafutwa (ila kazi hiyo ilizuiliwa kwa sababu bei ya tenda ilikuwa kubwa mara mbili zaidi ya bei za kawaida ndipo Serikali ikazuia tenda hiyo.)
Ndipo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya alilazimika kuomba kipaza sauti na kumwahidi Waziri Mkuu kwamba ndani ya mwezi huu tenda hiyo itakuwa imetangazwa.
Mapema asubuhi, Dkt. Mwigulu Nchemba alitembelea daraja la Nyathorogo lina urefu wa mita 36 na upana wa mita 7.6 ambalo linaunganisha wilaya za Rorya na Tarime. Daraja hilo limegharimu sh. milioni 729.
Meneja wa TARURA wa Wilaya ya Rorya, Mhandisi Elifadhili Moses alimweleza Waziri Mkuu kwamba daraja hilo limejengwa kwa teknolojia ya mawe iliyowezesha kupunguza nusu ya gharama za ujenzi na kwamba Serikali imetenga fedha katika mwaka ujao wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa kingo za mto ili kulinda daraja dhidi ya athari za maji.
“Awali, makadirio ya mradi huu yalikuwa shilingi bilioni 1.4 lakini kwa kutumia teknolojia hii ya mawe tumeweza kupunguza gharama kwa asilimia 50. Hivi sasa mradi huu uko katika muda wa uangalizi,” alisema.
Alisema kabla ya kujengwa kwa daraja hili, wananchi walilazimika kusafiri umbali wa km. 40 kutoka Utegi kwenda barabara kuu ya TANROADS lakini kupitia ujenzi wa daraja hilo, wananchi watasafiri km.10 tu kupitia Komeswa hadi kufika kwenye hiyo barabara kuu.
Naye, Mbunge wa Rorya, Bw. Jafari Chege alisema daraja hilo limeondoa adha ya muda mrefu iliyokuwa ikiwakabili wananchi wa Rorya na Tarime, ambapo awali walilazimika kuvuka Mto Nyathorogo katika mazingira hatarishi.
Alisema ujenzi wa daraja hilo umeboresha mawasiliano kati ya wilaya hizo mbili na kurahisisha usafirishaji wa mazao na unafuu wa kupeleka mazao kwenye soko lao kuu ambalo ni Tarime mjini.
