Na Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma

Kampuni ya Barrick inayofanya shughuli zake kwa ubia na Serikali kupitia Twiga Minerals imeahidi kuwa kupitia programu ya Barrick-Twiga Future Forward Education Program itaendelea kufanya kazi na Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha sekta ya elimu kwa kuimarisha miundombinu na kuwezesha mazingira rafiki ya kujifunzia ili kuchochea maendeleo ya taifa.

Akizungumza Julai 2,2026 na waandishi wa habari mara baada ya uzinduzi wa kitaifa wa awamu ya pili ya mradi huo, Meneja Mkazi wa Barrick nchini, Dkt. Melkiory Ngido, amesema kuwa baada ya makubaliano na Serikali mwaka 2023, Barrick ilikubali kutoa zaidi ya shilingi bilioni 70 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, mabweni na matundu ya vyoo katika shule za sekondari nchini.

Amesema kuwa mradi wa Barrick-Twiga Future Forward Education Program unalenga kuwekeza kwa Watanzania kwa kuweka mbele maslahi ya jamii kupitia uboreshaji wa miundombinu ya elimu ili kutengeneza mazingira bora zaidi ya kujifunza na kufundishia kwa walimu na wanafunzi.

Aidha, amebainisha kuwa awamu ya pili ya programu hiyo imezinduliwa kwa kujenga madarasa sita na mabweni mawili yenye madawati na vitanda kwa ajili ya wanafunzi wa kike wa kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Kibaigwa, mkoani Dodoma.

Pia ameongeza kuwa mradi huo unalenga kujenga madarasa 1,090, majengo ya maliwato na vyoo 1,640 pamoja na mabweni 270 katika shule 161 nchini kote ili kusaidia kuwapatia malazi wanafunzi takribani 190,000 wa kidato cha tano na sita.

Amesema kuwa Barrick ni mdau mkubwa katika sekta ya elimu baada ya kuingia makubaliano na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kutoa ufadhili wa shilingi bilioni 25 kwa ajili ya tafiti, uzalishaji wa wanataaluma na kuiwezesha sekta ya madini kupata wataalamu wenye maarifa.

Aidha, amesema kuwa tangu mwaka 2020 baada ya kuundwa kwa Twiga Minerals, Barrick imeendelea kushirikiana na Serikali katika kuendeleza sekta ya madini ili ilete tija na maendeleo endelevu nchini.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, amesema kuwa sekta ya elimu ina mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa na ustawi wa wananchi, hivyo ni muhimu miundombinu hiyo itunzwe na kulindwa kwa maslahi ya vizazi vijavyo.

Amesema kuwa anaishukuru Kampuni ya Barrick kwa uwekezaji huo katika sekta ya elimu na ana imani kuwa itaendelea kushirikiana na Serikali hata baada ya kukamilika kwa awamu ya pili ya mradi huo.

Aidha, amebainisha kuwa mazungumzo ya awali ya ushirikiano huo yalifunguliwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na jukumu lililobaki ni kuendeleza juhudi hizo.

Naye Meneja wa Fedha wa Barrick, Penina Kituku, amesema kuwa uwekezaji huo katika sekta ya elimu ni muhimu kwa kufungua fursa za elimu kwa Watanzania kupitia kuboresha mazingira ya kusomea na kujifunzia.

Pia ameongeza kuwa Barrick inajivunia kushiriki katika maendeleo ya sekta ya elimu nchini na itaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha watoto wa Kitanzania wanapata elimu katika mazingira bora na rafiki.

Kampuni ya Barrick inaendesha migodi ya Bulyanhulu iliyopo Kahama, North Mara iliyopo Tarime pamoja na mgodi wa Buzwagi uliopo Kahama ambao upo katika hatua za mwisho za kufungwa.