Na Mwandishi wetu,Mbinga
MKUU wa mkoa wa Ruvuma Ahmed Abbas,amezitaka halmashauri zote za mkoa huo kuhakikisha zinatoa elimu ya sheria ya urithi na mirathi kwa watoto na wajane ili waweze kufahamu na kulinda haki zao,kuwawezesha wajane kiuchumi kwa kuwapa mikopo ili kuongeza mitaji pamoja na kuwapa elimu ya ujasiriamali.
Abbas,ametoa agizo hilo jana kwenye hotuba yake iliyosomwa na mkuu wa wilaya ya Mbinga Kisare Makori katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wajane na siku ya mtoto wa afrika ambayo kimkoa imefanyika wilayani Mbinga.
Alisema,kulinda haki zao,kuheshimu utu wao na kuwawezesha kiuchumi huchangia moja kwa moja watoto kupata haki,malezi bora,elimu,afya na ulinzi unaostahili.
Aidha alisema,malezi bora ya watoto hayawezi kutenganishwa na ustawi wa wazazi na walezi wao kwani wajane wengi hubeba jukumu la kulea watoto pekee yao wakiwa katika mazingira yenye changamoto za kiuchumi,kijamii na kisheria.
“Tunapoadhimisha siku ya mtoto wa Afrika,tunakumbushwa kwamba kila mototo ana haki ya kuishi,kupata elimu bora,huduma za afya,lishe,ulinzi na malezi yanayomwezesha kukua katika mazingira salama,hivyo malezi bora yanaanzia ndani ya familia yakishirikisha wazazi,walezi,jamii na Serikali”alisema Abbas.
Alisema,mtoto anayelelewa katika mazingira ya upendo,maadili mema na ulinzi wa kutosha hukua akiwa raia mwema,mwenye uzalendo na uwezo wa kuchangia maendeleo ya Taifa.
Alieleza kuwa,Serikali inatambua na kuthamini wajane na watoto katika Taifa hili ndiyo maana imeweka mpango na mikakati mbalimbali ya kuhakikisha inawanua wajane kiuchumi na kukuza pato la familia na kaya kwa ujumla kwa kuwa ukimuinua mwanamke mmoja umeinua jamii nzima.
Alisema, Serikali imeendelea kutoa miongozo mbalimbali ikiwemo ya haki za watoto na ustawi wao ili kuwawezesha kiuchumi wajane kwa lengo la kuwasaidia kuongeza mitaji na kukuza uchumi wa kaya na Taifa kwa ujumla.
Abbas,ametoa wito kwa jamii,wadau wa maendeleo na familia kushirikiana na kuondoa ubaguzi,ukatili na vikwanzo vinavyowakabili watoto na wajane na kuendelea kuwekeza katika malezi chanya ya watoto na kuwawezesha wajane ili wajitegemee kiuchumi na waweze kutekeleza wajibu wa kulea familia katika mazingira salama na yenye heshima.
Mwenyekiti wa wajane wilaya ya Mbinga Eustella Mauga alisema,licha ya wajane kuwa sehemu muhimu katika jamii yetu na kuwa na mchango mkubwa katika malezi ya familia,amendeleo ya jamii na uchumi wa Taifa lakini bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali baada ya kufiwa na wenza wao.
Mauga ametaja baadhi ya changamoto zinazowakabili wajane ni kunyimwa haki za kurithi mali walizoachiwa na wenza wao,ukatili wa kijinsia,kurithiwa na ndugu za mume,umaskini,ukosefu wa mitaji ya kuanzisha au kuendeleza shughuli za kiuchumi na kukosa elimu ya kutosha kuhusu haki za kisheria.
Alisema,jamii inawaweka wajane katika kundi la watu wasiojiweza kutokana na mfumo dume,hata hivyo wanaendelea kupambana ili kujipatia kipato cha kukidhi mahitaji ya familia kwa kufanya shughuli mbalimbali kama vile kilimo,ufugaji na biashara ndogo ndogo.
“Sisi wanawake tumejipanga kutekeleza kwa vitendo Kauli mbiu hii ya mwaka 2026 Isemayo Imarisha Haki,Utu na Uwezeshaji kichumi kwa wajana,kauli mbiu hii inasisitiza umuhimu wa kuhakikisha wajane wanapata haki zao za msingi,wanaheshimiwa na kuthaminiwa katika jamii”alisema Mauga.
Kwa upande wake Afisa ustawi wa jamii wa Halmashauri ya wilaya Mbinga Filbert Mahay alisema,Halmashauri za wilaya Mbinga zinaendelea na jitihada mbalimbali katika kulinda na kutetea haki za mtoto ikiwemo utoaji elimu kwa jamii na shuleni.
Alisema,Serikali kupitia Halmashauri ya Mji Mbinga na Mbinga vijijini zinachukua hatua kuhusu ukiukwaji wa haki za mtoto,upatikanaji wa huduma za afya na utoaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano na kuimarisha usalama wa watoto mashuleni.
“kwa kipindi cha mwaka 2026 jumla ya shule za msingi 29 na shule za sekondari 14 wilayani Mbinga,zimefikiwa na huduma ya elimu kuhusu ukatili dhidi ya watoto na wanafunzi 7004 waliweza kufikiwa na kupata elimu dhidi ya vitendo vya ukatili”

