Na.Sophia Kingimali.
Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limetangaza utoaji wa huduma za haraka kwa wananchi katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), likiwataka waliopoteza vyeti na wanaohitaji huduma za ulinganifu wa sifa za elimu kutumia fursa hiyo.
Akizungumza katika maonesho hayo, Afisa Uhusiano wa NECTA, John Nchimbi, alisema baraza hilo linashiriki maonesho kuanzia Juni 28 hadi Julai 13 likitoa huduma mbalimbali zinazolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
Alisema huduma kubwa zinazotolewa ni pamoja na maombi ya vyeti mbadala kwa waliopoteza vyeti vyao pamoja na huduma ya ulinganifu wa vyeti kwa watu waliosoma nje ya Tanzania au katika mifumo ya elimu isiyotumia mtaala wa Tanzania.
Nchimbi alisema kwa utaratibu wa kawaida, mwombaji wa cheti mbadala hulazimika kusubiri hadi siku 30 kukamilisha mchakato, lakini katika maonesho ya Sabasaba huduma hiyo itatolewa ndani ya siku moja au mbili endapo mwombaji atawasilisha nyaraka zote zinazohitajika.
Amefafanua kuwa mwombaji wa cheti mbadala anatakiwa kuwa na tangazo la gazeti la kupoteza cheti, taarifa ya polisi (Loss Report), picha ya pasipoti pamoja na nakala ya kitambulisho.
Kwa upande wa waombaji wa ulinganifu wa vyeti, alisema wanapaswa kuwasilisha cheti walichopata kutoka nchi au bodi husika ya mitihani, kitambulisho pamoja na picha ya pasipoti ili huduma hiyo itolewe kwa haraka.
Aidha, aliwahimiza wananchi ambao wamekuwa wakisubiri kupata huduma hizo kwa muda mrefu kutumia maonesho hayo kwani yamekusudiwa kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.
Nchimbi alisema banda la NECTA linapatikana katika Banda la Jakaya Kikwete ndani ya viwanja vya Sabasaba, ambako wataalamu wa baraza hilo wanapatikana kutoa msaada, ushauri na kupokea maombi mbalimbali.
Pia alitangaza kuwa usajili wa watahiniwa wa kujitegemea wa Mtihani wa Kidato cha Sita unaanza rasmi Julai Mosi, huku waombaji wote wakihimizwa kufuata taratibu zilizowekwa.
Alisema watahiniwa wanaotaka kufanya mtihani wa kujitegemea au wanaorudia mtihani wanaweza kutembelea banda la NECTA kupata maelekezo ya usajili na msaada wa namna ya kukamilisha maombi yao.
Aliongeza kuwa maafisa wa NECTA waliopo katika maonesho hayo wamejipanga kuhakikisha kila mwananchi anayefika anapata huduma kwa wakati na bila usumbufu.
Nchimbi alitoa wito kwa wananchi kutumia kikamilifu siku za maonesho ya Sabasaba kutembelea banda la NECTA ili kupata huduma mbalimbali za elimu kwa urahisi na kwa muda mfupi kuliko ilivyo katika utaratibu wa kawaida.

