Na. John Bukuku – Dar Es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa uwekezaji wenye matokeo ni ule unaovutia mitaji, kupunguza gharama za kufanya biashara, kukuza ajira, kuimarisha huduma, kuongeza mapato ya Serikali na kulinda maslahi ya wananchi, akibainisha kuwa huo ndio uwekezaji wenye tija.
Amesema hayo Juni 30, 2026 wakati akipokea gawio na michango kutoka kwa viongozi wa taasisi na mashirika ya umma, kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, iliyoambatana na kauli mbiu isemayo “Uwekezaji wa Umma wenye Matokeo: Nguzo ya Uchumi Shindani na Maendeleo Endelevu Kuelekea Dira 2050”
Aidha amebainisha kuwa ili kauli mbiu hiyo ipate maana na uhalisia lazima itafsiriwe katika mipango ya kazi na huduma zinazomfikia mwananchi.
Amesisitiza kuwa kila shirika, taasisi na wizara lazima zitafsiri kauli mbiu hiyo kwenye kazi zao ili kufikisha huduma njema kwa wananchi na kukuza uchumi wa nchi.
Huku akibainisha kuwa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya 2050 unahitaji taasisi zenye uwezo wa kuingia kwenye ushindani wa soko, aidha amebainisha kuwa kuanzia Julai Mosi 2026 inapoanza utekelezaji wa Dira ya 2050 taasisi na mashirika zinatakiwa kuwa makini, huku akitoa rai kwa mashirika na taasisi ambazo bado zinasuasua zijitathmini.
Aidha amesikitishwa na mikopo mingine inayokopwa pasipokuwa na tija yoyote kwa Serikali, huku akibainisha kuwa Serikali inahitaji taasisi zinazotumia teknolojia na zinazopunguza upotevu wa mali, zinazovutia mitaji na kufungua fursa kwa sekta binafsi.
Aidha amebainisha kuwa Serikali haifanyi kazi peke yake, ni muhimu kufungua fursa kwa sekta binafsi ziingie, akibainisha kuwa sekta binafsi ni mshirika mkubwa kwenye maendeleo.

