Mratibu wa Uchumi Parachichi Marathon Respicius Mtabingwa 

DENIS MLOWE ,NJOMBE 

JUMLA ya shilingi milioni 32.96 zinatarajiwa kutolewa kwa washindi wa mashindano ya Uchumi Parachichi Marathon 2026 yatakayofanyika Agosti 23, 2026 mkoani Njombe, katika tukio linalolenga kuhamasisha michezo, afya na ukuaji wa uchumi kupitia zao la parachichi.

Mashindano hayo yatahusisha mbio za kilomita 42, 21 na 10 kwa wanaume na wanawake pamoja na mbio za watoto, huku washindi wa nafasi mbalimbali wakijizolea zawadi za fedha taslimu.

Akizungumza na Full Shangwe kuhusu maandalizi ya tukio hilo, Mratibu wa Uchumi Parachichi Marathon, Respicius Mtabingwa, alisema marathon hiyo imeandaliwa kwa lengo la kuunganisha michezo na shughuli za kiuchumi zinazohusiana na zao la parachichi ambalo lina mchango mkubwa katika maisha ya wananchi wa Mkoa wa Njombe.

“Tunataka kutumia michezo kama njia ya kuitangaza Njombe na fursa zilizopo katika sekta ya parachichi. Hii siyo tu mbio za kukimbia, bali ni jukwaa la kuonesha uwezo wa wakulima wetu na mchango wa zao hili katika uchumi wa mkoa na taifa,” alisema Mtabingwa.

Aliongeza kuwa tukio hilo linatarajiwa kuvutia washiriki na wageni kutoka maeneo mbalimbali nchini, jambo litakaloongeza fursa za biashara, utalii na uwekezaji katika Mkoa wa Njombe.

MtMtabingwalisema kuwa washindi wa kwanza wa mbio za kilomita 42 kwa upande wa wanaume na wanawake atazawadiwa shilingi milioni tatu, huku washindi wa nafasi nyingine wakipata zawadi kulingana na viwango vilivyopangwa katika kila kundi la mbio.

Washiriki wa marathon hiyo watatakiwa kulipa ada ya usajili ya shilingi 35,000 kwa watu wazima na shilingi 20,000 kwa watoto, ambapo kila mshiriki atapatiwa fulana na medali ya ushiriki.

Marathon hiyo inatarajiwa kuwa miongoni mwa matukio makubwa ya michezo ya mwaka 2026 katika Mkoa wa Njombe, huku ikitumika kama jukwaa la kuhamasisha uzalishaji, biashara na matumizi ya zao la parachichi nchini.