Na Mwandishi Wetu, Songea 

Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imeendesha mafunzo ya siku moja kwa vijana, wafanyabiashara, wakandarasi, watoa huduma na wadau wa ununuzi wa umma pamoja na makundi maalum wa mkoa wa Ruvuma na kuwasihi kutumia kikamilifu fursa zinazopatikana katika zabuni za Umma.

Mafunzo hayo yaliyofanyika katika Halmashuri ya Manispaa ya Songea tarehe 18 Juni 2026 yamelenga kuongeza uelewa juu ya Fursa na Haki za Vijana, Wafanyabiashara na Makundi Maalum katika kushiriki Mchakato wa Ununuzi wa Umma.

Akifungua Mafunzo hayo, kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Bw. Jumanne Mwankhoo amesema kuwa Serikali ya awamu ya Sita imeweka mazingira bora ya kuwainua wananchi kiuchumi kupitia mifumo ya ununuzi wa umma inayowezesha wazabuni kushiriki kwa uwazi huku haki zao zikilindwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za Ununuzi wa Umma nchini.

Bw. Mwankhoo ameipongeza PPAA kwa kuendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara, vijana na makundi maalum kuhusu fursa zilizopo katika zabuni za umma ikiwa ni njia ya kuwawezesha vijana na makundi maalum kupata uelewa wa sheria za ununuzi wa umma, haki zao pamoja na namna bora ya kushiriki katika zabuni za Serikali.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mtendaji wa PPAA, Bw. Paschal Kajuna amesema lengo la mafgunzo hayo ni kuongeza uelewa wa Vijana, wafanyabiashara na makundi maalum kuhusu haki zao katika michakato ya ununuzi wa umma pamoja na matumizi ya mifumo ya kidijitali katika kushughulikia malalamiko na rufaa.

Bw. Kajuna amesema kuwa matumizi ya Moduli ya kushughulikia Malalamiko na Rufaa katika mfumowa NeST yameleta manufaa mbalimbali ikiwemo kuokoa muda, kupunguza gharama, kuongeza uwazi na uwajibikaji pamoja na kuweka kumbukumbu sahihi za malalamiko na rufaa zinazowasilishwa na wazabuni.

Kwa mwaka wa fedha 2025/26, PPAA imefanikiwa kutoa elimu kwa wazabuni 1,717 pamoja na watumishi 705 wa idara za ununuzi na sheria katika maeneo mbalimbali nchini.

Kadhalika, Bw. Kajuna amewataka vijana kuchangamkia fursa za mafunzo zinazotolewa na PPAA ili waweze kunufaika na Fursa na Haki za Vijana, Wafanyabiashara na Makundi Maalum katika kushiriki Mchakato wa Ununuzi wa Umma.

PPAA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) imeendesha mafunzo hayo ya siku moja yamehudhuriwa na washiriki takribani 200 kutoka Wilaya za mkoa wa Ruvuma.

Aidha, mafunzo hayo ni mwendelezo wa mafunzo yaliyopkuwa yakitolewa na PPAA kwa Kanda za Pwani, Ziwa, Kaskazini, Nyanda za Juu Kusini na Mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Mbeya, Iringa, Njombe na Ruvuma.