Na Mwamvua Mwinyi, Mafia

Zaidi ya wananchi 2,000 wamejitokeza kupata huduma katika kambi ya matibabu ya madaktari bingwa na wabobezi iliyoandaliwa na Taasisi ya Jamii Bora kwa ufadhili wa Benki ya Amana kupitia Mfuko wake wa Hisani, tangu Juni 15 hadi 19, 2026.

Kambi hiyo imekuwa mkombozi kwa wakazi wa Wilaya ya Mafia kwa kuwawezesha kupata huduma za kibingwa ambazo kwa kawaida hulazimika kusafiri umbali mrefu kuzifuata.

Akizungumza wakati wa kuwapokea viongozi wa Benki ya Amana na wadau wengine wa kambi hiyo Juni 18, 2026, Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Aziza Mangosongo, alisema ujio wa madaktari bingwa zaidi ya 60 umeiwezesha jamii kupata huduma za afya za kibingwa ambazo si rahisi kupatikana kwa wakati mmoja wilayani humo.

Alisema wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo, ikiwemo Jibondo, Chole, Juani, Kanga na Baleni, wamepata huduma za matibabu ya magonjwa mbalimbali yakiwemo ya macho, masikio, uzazi, watoto, wazee pamoja na magonjwa mengine bila kulipia gharama yoyote.

Pia alitoa wito kwa wadau hao kuendelea kuandaa kambi kama hizo mara kwa mara ili kuwafikia wananchi wengi zaidi wenye uhitaji wa huduma za afya za kibingwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Amana, Abubakar Othman Ali, alisema taasisi hiyo imeridhishwa na mwitikio mkubwa wa wananchi pamoja na ubora wa huduma zinazotolewa katika kambi hiyo.

“Hii ni kambi ya tano tangu tuanze mkakati huu wa kusogeza huduma za madaktari bingwa kwa wananchi, na tutaendelea kufikia maeneo mengine yenye uhitaji kama huu,” alieleza.

Vilevile alitoa wito kwa wadau wengine kuungana na Benki ya Amana na Taasisi ya Jamii Bora katika kusogeza huduma za afya kwa wananchi, huku akiipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha mazingira ya sekta ya afya nchini.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia, Mussa Kitungi, alisema halmashauri hiyo ipo tayari kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika sekta za afya, elimu na maendeleo kwa lengo la kuboresha ustawi wa wananchi wa Wilaya ya Mafia.