Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo, Balozi Stephen Mbundi akizungumza kwenye hafla hiyo jijini Arusha .
………
Na Happy Lazaro,Arusha .
SERIKALI ya Ujerumani imeendelea kuimarisha ushirikiano wake na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa kutoa msaada wa zaidi ya Euro milioni 8 kwa ajili ya kuimarisha sekta ya afya na kukabiliana na milipuko ya magonjwa ya kuambukiza katika ukanda huo.
Msaada huo umetangazwa katika Makao Makuu ya Sekretarieti ya EAC jijini Arusha wakati wa mkutano uliowakutanisha viongozi wa jumuiya hiyo, wawakilishi wa Serikali ya Ujerumani pamoja na wadau wa vyombo vya habari.
Akizungumza kwenye hafla hiyo iliyofanyika makao makuu ya EAC ,Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo Balozi Stephen Mbundi amesema kuwa ,Benki ya Maendeleo ya KfW kwa niaba ya Serikali ya Ujerumani imesaini makubaliano ya kutoa Euro milioni 5 zitakazotumika kuimarisha sekta ya afya ya kikanda katika kukabiliana na ugonjwa wa Mpox na milipuko mingine ya magonjwa hatari ya kuambukiza.
“Fedha hizo pia zitalenga kuboresha uwezo wa maabara katika nchi wanachama wa EAC ili kuwezesha uchunguzi wa haraka wa magonjwa na kuongeza uwezo wa kukabiliana na dharura za afya ya umma.”amesema Balozi Mbundi.
Amesema kuwa mbali na msaada huo, Serikali ya Ujerumani imeahidi kutoa Euro milioni 3 zaidi kupitia KfW kwa ajili ya kusaidia juhudi za kukabiliana na ugonjwa wa Ebola ambao umeendelea kuwa tishio katika baadhi ya maeneo ya ukanda wa Afrika Mashariki.
Ameongeza kuwa, EAC itapokea seti 500 za vifaa kinga binafsi (PPEs) vitakavyotumika kuwasaidia wahudumu wa afya waliopo mstari wa mbele katika shughuli za maandalizi na mwitikio dhidi ya milipuko ya magonjwa.
“Ushirikiano kati ya jumuiya hiyo na Serikali ya Ujerumani umeendelea kuleta matokeo chanya katika kuimarisha mifumo ya afya na ustahimilivu wa nchi wanachama dhidi ya majanga ya kiafya.”amesema Balozi Mbundi.
“Tunathamini sana ushirikiano wa muda mrefu na Serikali ya Ujerumani ambao umeendelea kuimarisha uwezo wetu wa kukabiliana na changamoto za afya ya umma. Msaada huu utaongeza uwezo wa nchi wanachama kuzuia, kugundua na kudhibiti milipuko ya magonjwa kwa wakati,” amesema.
Ameongeza kuwa ,kupitia msaada wa Ujerumani, EAC imefanikiwa kupeleka maabara 10 zinazohamishika katika nchi saba wanachama ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, hatua iliyosaidia kuimarisha huduma za uchunguzi wa haraka wa magonjwa.
“Maabara hizo zimekuwa na mchango mkubwa katika kukabiliana na milipuko mbalimbali ikiwemo UVIKO-19, Ebola nchini Uganda mwaka 2022, Marburg nchini Tanzania mwaka 2023 na Mpox mwaka 2024, huku EAC ikisisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo kujenga Afrika Mashariki yenye afya bora, salama na yenye uwezo mkubwa wa kukabiliana na changamoto za afya za sasa na zijazo.”amefafanua Balozi huyo.
