NA DENIS MLOWE, IRINGA
MKUU wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amesema Mkoa wa Iringa unaendelea kuwa moja ya maeneo bora kwa uwekezaji nchini kutokana na mazingira mazuri ya biashara, hali ya hewa rafiki, upatikanaji wa rasilimali, miundombinu imara pamoja na nguvu kazi ya kutosha.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Iringa Shopping Mall, Kheri James alisema mkoa huo una sifa nyingi zinazowavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, huku akiwataka wananchi kuwa mabalozi wa kuhamasisha uwekezaji zaidi ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
Alisema miongoni mwa sababu zinazoufanya mkoa wa Iringa kuwa kitovu muhimu cha uwekezaji ni hali nzuri ya hewa inayomwezesha mtu yeyote kuishi na kufanya shughuli zake bila changamoto kubwa, pamoja na uwepo wa rasilimali mbalimbali ambazo hazipatikani kwa urahisi katika maeneo mengine ya nchi.
“Mkoa wa Iringa una watu wanaopenda kazi na wana uwezo mkubwa wa kufanya kazi. Hivyo mwekezaji anayehitaji nguvu kazi katika viwanda, biashara au sekta ya huduma anaweza kuipata kwa urahisi hapa Iringa,” alisema.
Aidha, alibainisha kuwa upatikanaji wa maji ya uhakika na mtandao wa barabara unaofikika kwa urahisi ni miongoni mwa mambo yanayochochea ukuaji wa uwekezaji katika mkoa huo.
Kheri James alisema Iringa bado ina nafasi kubwa ya biashara na huduma, jambo linalowapa fursa wawekezaji wapya kuanzisha shughuli zao bila kukutana na ushindani mkubwa.
Aliwataka wananchi kuendelea kuwahamasisha wawekezaji kuja kuwekeza mkoani humo na wakati huo huo kuunga mkono uwekezaji kwa kununua na kutumia bidhaa zinazotokana na miradi ya uwekezaji inayotekelezwa ndani ya mkoa.
Katika hafla hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa aliwapongeza wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, menejimenti pamoja na wafanyakazi wa Iringa Shopping Mall kwa kuamua kuwekeza Iringa, akieleza kuwa uwekezaji huo utarahisisha upatikanaji wa bidhaa na huduma kwa wananchi.
Alisema kabla ya uwepo wa kituo hicho kikubwa cha biashara, wananchi wengi walilazimika kusafiri hadi Dar es Salaam kufuata baadhi ya bidhaa na huduma, hali ambayo sasa itapungua kwa kiasi kikubwa kutokana na uwepo wa Iringa Shopping Mall.
“Uwekezaji huu utasaidia wananchi kupata bidhaa karibu yao, utazalisha ajira kwa vijana na kuchochea ukuaji wa biashara ndani ya mji wa Iringa. Pia utawasaidia wafanyabiashara wadogo kupata bidhaa kwa urahisi na kwa gharama nafuu zaidi,” alisema.
Kheri James aliahidi kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kuhakikisha usalama unaimarishwa, huduma muhimu zinaendelea kuboreshwa na changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa miradi ya uwekezaji zinatatuliwa kwa wakati.
Alisema Serikali ya Mkoa itaendelea kushirikiana na wawekezaji ili kuhakikisha miradi yote inayowekwa Iringa inafanya kazi kwa ufanisi na kuchangia maendeleo ya wananchi.
Alisema bado kuna maeneo mengi ya uwekezaji yanayohitaji kuendelezwa Iringa, akitolea mfano miradi ya majengo ya biashara inayotekelezwa na kampuni mbalimbali pamoja na taasisi za nyumba nchini.
Aliwahimiza wawekezaji kutumia fursa zilizopo mkoani humo, akisisitiza kuwa Iringa ni lango muhimu la ukanda wa Nyanda za Juu Kusini na eneo lenye mchango mkubwa katika shughuli za kiuchumi za taifa.
“Ukiipata Iringa umeipata Nyanda za Juu Kusini, na ukiipata Iringa umepata soko kubwa la biashara na huduma. Hivyo ni wakati wa kuchangamkia fursa zilizopo kwa ajili ya maendeleo ya mkoa wetu na taifa kwa ujumla,” alisema.

