Na Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM anayeshughulikia Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Ndugu Kenani Kihongosi, amesema kuwa chama hicho kimepata taarifa zinazoashiria kuwepo kwa vikao vya siri vinavyodaiwa kufanywa na baadhi ya viongozi wa Chama Fulani kwa lengo la kuhamasisha maandamano na vurugu nchini.

Akizungumza Juni 13, 2026 na waandishi wa habari jijini Dodoma, Kihongosi amesema kuwa taarifa walizonazo zinaonyesha baadhi ya wanasiasa na wanaharakati wamekuwa wakiratibu ajenda za maandamano badala ya kushiriki katika mijadala ya maendeleo inayowanufaisha wananchi.

Aidha, amebainisha kuwa viongozi wa kisiasa wanapaswa kuelekeza nguvu zao katika kujenga taifa kupitia hoja na sera zenye manufaa kwa wananchi badala ya kushawishi vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani na usalama.

Amesema kuwa Watanzania wanahitaji majibu ya changamoto zao za kila siku, hivyo siasa zinapaswa kujengwa katika msingi wa ushindani wa sera na hoja za maendeleo.

Kihongosi ameongeza kuwa CCM itaendelea kuweka mkazo katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayogusa sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, maji na miundombinu kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi.

Pia amesema kuwa viongozi wa chama hicho wamekuwa wakifanya ziara katika maeneo mbalimbali nchini kusikiliza kero za wananchi na kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili.

Aidha, amewataka wananchi kutoshabikia maandamano na vurugu kwa namna yoyote ile, akieleza kuwa mara nyingi athari zake huwakumba zaidi wananchi wa kawaida wakiwemo wafanyabiashara wadogo, mama lishe, waendesha bodaboda na vijana wanaojitafutia kipato.

Amebainisha kuwa umoja wa kitaifa, amani na mshikamano ni nguzo muhimu za maendeleo ya nchi, hivyo Watanzania wanapaswa kuendelea kuvilinda bila kujali tofauti zao za kisiasa au kijamii.

Kihongosi amesema kuwa tofauti za kimtazamo zinapaswa kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo na kuheshimiana ili kuendelea kudumisha utulivu wa taifa.

Sambamba na hilo, amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea kuwa macho dhidi ya viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani, huku akiwataka wananchi kushirikiana navyo kwa kutoa taarifa mapema.

Akizungumzia Bajeti ya Serikali iliyowasilishwa bungeni hivi karibuni, Kihongosi amesema kuwa imeonyesha hatua kubwa ya kuimarisha uchumi wa nchi na kujitegemea kifedha, huku akiipongeza Serikali pamoja na Bunge kwa kusimamia mipango ya maendeleo inayolenga ustawi wa wananchi.