Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Dkt. Bill Kiwia, amesema ushirikiano wa waajiri katika kuwasilisha taarifa za waajiriwa wapya na marejesho ya mikopo kwa wakati umeendelea kuimarisha mfuko wa mikopo na kuongeza uwezo wa kuwafikia wanafunzi wengi zaidi wanaohitaji msaada wa kifedha kwa ajili ya elimu ya juu.
Dkt. Kiwia amesema hayo Juni 12, 2026 wakati wa hafla fupi ya utoaji tuzo kwa waajiri wanaozingatia Sheria ya HESLB iliyofanyika katika ofisi za HESLB Kanda ya Mashariki jijini Dar es Salaam, ambapo waajiri 11 kutoka mikoa ya Dar es Salaam na Pwani walitambuliwa kwa kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria.
Amesema waajiri hao wamekuwa mfano wa kuigwa kwa kuwasilisha kwa wakati taarifa za waajiriwa wapya pamoja na kuhakikisha makato ya marejesho ya mikopo yanawasilishwa HESLB kwa mujibu wa sheria baada ya kuthibitishwa kuwa waajiriwa hao ni wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu.
“Tumekusanyika hapa si kwa ajili ya kutoa tuzo pekee, bali pia kutambua mchango mkubwa wa waajiri katika kufanikisha dhamira ya Taifa ya kuwekeza katika elimu kupitia mikopo ya elimu ya juu,” amesema Dkt. Kiwia.
Amesema kila mwajiri anayewasilisha taarifa za waajiriwa wapya kwa wakati na kila shilingi inayorejeshwa HESLB ina mchango mkubwa katika kutimiza ndoto za vijana wengine wanaotamani kupata elimu ya juu lakini wanakabiliwa na changamoto za kifedha.
Kwa mujibu wa Dkt. Kiwia, fedha zinazorejeshwa na wanufaika wa mikopo hutumika kusaidia wanafunzi wengine wapya wenye sifa na uhitaji wa kifedha, jambo linaloufanya mfumo wa mikopo kuwa endelevu kwa vizazi vijavyo.
Aidha, amesema mahitaji ya elimu ya juu nchini yanaendelea kuongezeka sambamba na ongezeko la wanafunzi wanaohitimu elimu ya sekondari, hali inayoongeza umuhimu wa ukusanyaji wa marejesho ya mikopo ili kuiwezesha Serikali kugharimia wanafunzi wengi zaidi.
Akizungumzia hali ya makusanyo ya mikopo, Dkt. Kiwia amesema mwaka 2022/2023 HESLB ilikusanya shilingi bilioni 169, mwaka 2023/2024 zilikusanywa shilingi bilioni 177 huku mwaka 2024/2025 kiasi cha shilingi bilioni 194.5 kikikusanywa.
Ameongeza kuwa hadi Mei 31, 2026, HESLB ilikuwa imekusanya shilingi bilioni 215.6 sawa na asilimia 98 ya lengo la mwaka la kukusanya shilingi bilioni 220, akieleza kuwa mwenendo huo unaonesha uwezekano wa kuvunjwa kwa rekodi mpya ya ukusanyaji wa zaidi ya shilingi bilioni 200 kwa mwaka.
“Mafanikio haya kwa kiasi kikubwa yanatokana na mchango mkubwa wa waajiri wanaotambua umuhimu wa kurejesha fedha hizi kwa wakati ili kuiongezea Serikali uwezo wa kuwafikia wanafunzi wengi zaidi,” amesema.
Katika kuongeza ufanisi wa marejesho ya mikopo, Dkt. Kiwia amesema HESLB imeendelea kuboresha mifumo ya kidijitali kwa ajili ya kurahisisha utambuzi wa wanufaika, usimamizi wa marejesho na upatikanaji wa taarifa za waajiri na wanufaika kwa wakati.
Pia amesema HESLB imeendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi mbalimbali zikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania, Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa pamoja na kampuni ya CreditInfo Tanzania ili kubaini kwa haraka wanufaika walioajiriwa na kuhakikisha marejesho yanaanza kwa wakati.
Amesema hatua ya kuunganisha mifumo ya taarifa za Serikali inaendana na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, aliyesisitiza mifumo ya Serikali kusomana ili kuongeza ufanisi wa utoaji huduma, kudhibiti mianya ya rushwa na kuongeza ukusanyaji wa mapato.
Akihitimisha hotuba yake, Dkt. Kiwia aliwashukuru waajiri, wanahabari na wadau mbalimbali kwa kuendelea kushirikiana na HESLB katika utekelezaji wa sheria, huku akiwapongeza washindi wa tuzo hizo na kuwataka kuendelea kuwa mabalozi wa uzingatiaji wa sheria katika taasisi zao na kwa waajiri wengine nchini.

