NA FAUZIA MUSSA
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imepongeza kurejea kwa Klabu ya Lions Zanzibar baada ya kusitisha shughuli zake kwa zaidi ya miaka 26, ikieleza kuwa taasisi za kijamii na misaada ya kibinadamu zina mchango mkubwa katika kusaidia juhudi za maendeleo na ustawi wa wananchi.
Akifungua rasmi Klabu ya Lions Zanzibar Stone Town katika ukumbi wa Maru Maru, Mjini Unguja, Naibu Waziri wa Vijana, Ajira na Uwezeshaji, Hassan Khamis Hafidh, alisema uwepo wa taasisi zinazojihusisha na huduma za jamii husaidia serikali kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.
Alisema kufufuliwa kwa klabu hiyo kunakuja wakati muafaka ambapo serikali inaendelea kuimarisha ustawi wa jamii kupitia sekta za afya, elimu, uwezeshaji wa vijana na huduma za kijamii.
“Ushirikiano kati ya serikali na taasisi za kujitolea ni muhimu katika kuleta maendeleo endelevu na kuwafikia wananchi wenye mahitaji maalumu katika jamii,” alisema.
Kwa upande wake, Rais wa Klabu ya Lions Zanzibar Stone Town, Dk. Ameesh Mehta, alisema kurejea kwa klabu hiyo ni mwanzo wa safari mpya ya kuendeleza urithi wa huduma kwa jamii uliokuwepo Zanzibar miaka mingi iliyopita.
“Huu si uzinduzi wa klabu mpya pekee, bali ni kuzaliwa upya kwa dhamira ya kuhudumia jamii. Tunarejesha roho ya Lionism kwa lengo la kusaidia wananchi katika maeneo ya afya, elimu, mazingira na uwezeshaji wa vijana,” alisema.
Dk. Mehta alibainisha kuwa klabu hiyo ni sehemu ya mtandao mkubwa wa Lions Clubs International unaofanya kazi katika nchi nyingi duniani, na kwamba Zanzibar itanufaika na uzoefu na rasilimali za taasisi hiyo katika kutekeleza miradi ya maendeleo.
Naye, Gavana wa District wa Lions Clubs International Tanzania, Manish Chavda, alisema mafanikio ya huduma za kijamii yanahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali, akisisitiza kuwa tawi la Zanzibar litakuwa chachu ya mabadiliko chanya katika jamii.
Mmoja wa wanachama wa klabu hiyo aliwaomba wananchi, wafanyabiashara na taasisi mbalimbali kuunga mkono juhudi za kujitolea ili kuongeza wigo wa kuwafikia watu wenye uhitaji.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa klabu hiyo, Dipak Joshi, alisema wanachama wamejipanga kuhakikisha shughuli za misaada zinakuwa endelevu na zenye matokeo chanya kwa jamii.
Makamu wa Pili wa Rais, Sapna Brahmaroutu, alisisitiza umuhimu wa elimu katika maendeleo ya jamii, akieleza kuwa uwekezaji katika elimu ni msingi wa kujenga kizazi chenye uwezo wa kuleta mabadiliko ya kudumu.
Klabu ya Lions Zanzibar Stone Town imefadhiliwa na Lions Club ya Dar es Salaam Humanity na inalenga kuwa jukwaa muhimu la kujitolea, mshikamano na maendeleo endelevu kwa wananchi wa Zanzibar.
Klabu hiyo iliyoanzishwa zaidi ya miaka 100 iliyopita duniani, sasa imeanza rasmi safari mpya Zanzibar kwa dhamira ya kuwahudumia makundi mbalimbali yenye uhitaji na kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi visiwani hapa.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na viongozi wa Lions Clubs International, wafanyabiashara, wanachama wa diaspora pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo, ambapo zaidi ya shilingi milioni 30 zilikusanywa katika hafla hiyo kwa ajili ya kusaidia shughuli za kijamii.

