NA DENIS MLOWE IRINGA
SERIKALI imeeleza dhamira yake ya kuendelea kuimarisha michezo na sanaa shuleni kwa lengo la kuibua vipaji, kukuza ajira na kuandaa kizazi chenye uwezo wa kushindana kimataifa.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Profesa Riziki Shemdoe, wakati akimwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uzinduzi wa mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA Kitaifa 2026 uliofanyika kwenye Viwanja vya Kichangani mkoani Iringa.
Profesa Shemdoe alisema kuwa mashindano hayo si tukio la kawaida la michezo pekee bali ni sehemu muhimu ya mkakati wa taifa wa kujenga vijana wenye afya bora, nidhamu, uzalendo, kujiamini na uwezo wa kushindana katika mazingira ya kitaifa na kimataifa.
Alisema kaulimbiu ya mwaka huu ya “Michezo na Sanaa Shuleni, Daraja la Ajira, Afya na Ushindani wa Kimataifa” inaakisi nafasi kubwa ya michezo katika maendeleo ya vijana na uchumi wa taifa.
“Tunawapongeza wanamichezo wote kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar kwa kufika hapa Iringa salama. Mashindano haya ni chuo cha malezi ya vijana na msingi wa kujenga taifa la watu wanaojiamini, wanaowajibika na wenye moyo wa kushindana kwa haki,” alisema.
Aliiongeza kuwa Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya michezo katika shule na taasisi za elimu, kuimarisha uratibu wa michezo na sanaa, pamoja na kuhamasisha uwekezaji katika vituo vya kukuza vipaji na akademia za michezo.
Profesa Shemdoe alisema dunia ya sasa imeifanya michezo na sanaa kuwa taaluma na chanzo kikubwa cha ajira, hivyo kuna haja ya kuendelea kuwekeza katika sekta hizo ili kuwajengea vijana fursa za maendeleo.
Aidha, aliagiza kila halmashauri nchini kuwa na shule maalumu ya kukuza vipaji vya michezo na sanaa, kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya maendeleo ya sekta hiyo pamoja na kulinda maeneo yote yaliyotengwa kwa michezo.
Pia alielekeza kuanzishwa kwa mfumo wa kitaifa wa kutambua, kusajili na kuendeleza vipaji vya wanafunzi vinavyoibuka kupitia mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA ili kuhakikisha hakuna kipaji kinachopotea.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, alisema mkoa huo umejipanga kikamilifu kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika kwa mafanikio makubwa huku washiriki wote wakipata mazingira bora na salama.
Alisema Iringa imepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa mashindano hayo kwa mwaka wa pili mfululizo na inalenga kuandika historia nzuri katika usimamizi wa michezo hiyo ya kitaifa.
“Mkoa wetu umejiandaa vizuri kuhakikisha viwanja vinakuwa katika hali bora, usalama wa washiriki unaimarishwa na huduma zote muhimu zinapatikana kwa wakati,” alisema.
Kheri alisema wananchi wa Iringa wameandaliwa kuwakaribisha wageni kutoka mikoa yote ya Tanzania kwa ukarimu mkubwa na kuhakikisha wanapata huduma bora wakati wote wa mashindano.
Alisisitiza kuwa hali ya usalama na afya katika mkoa huo ni nzuri na kwamba washiriki wote watakuwa salama katika kipindi chote cha mashindano.
James alisema taasisi mbalimbali za michezo, makampuni na wadau wa maendeleo ya vipaji wamejitokeza kushuhudia mashindano hayo kwa lengo la kubaini na kusaidia kukuza vipaji vya vijana vinavyooneshwa katika mashindano hayo.
Mashindano ya UMITASHUMTA mwaka huu yanawakutanisha wanafunzi 3,417 pamoja na walimu 905 kutoka maeneo mbalimbali nchini, huku mashindano ya UMISSETA yanatarajiwa kuwakutanisha zaidi ya wanafunzi 3,400 pamoja na walimu na viongozi wa michezo takribani 900.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kuibua vipaji, kuimarisha umoja wa kitaifa na kuandaa kizazi cha vijana watakaoitangaza Tanzania katika michezo na sanaa ndani na nje ya nchi.

