MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amesema ziara ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan inathibitisha dhamira CCM nchi kutofungamana na upande wowote.
Amesema waasisi wa taifa wakiongozwa na Mwalimu Julius Nyerere, waliitaka Tanzania kuwa katikati pale pande mbili zinapogombana ili kuleta amani, umoja na kusikilizana.
Wasira alisema hayo akihitimisha Ziara yake wilayani Same Mkoa wa Kilimanjaro alipokuwa akizungumza Juni 9, 2026 na wana CCM na wananchi katika ziara ya kukagua uhai wa Chama na utekelezeji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
“Tulitaka tuwe huru na uhuru uwe wa kudumu, kwa hiyo kazi yetu ni kudumisha uhuru na kudumisha uhuru ni kutupa haki ya kuamua mambo tunayoona yanatufaa sisi sio kutegemea wengine wawaambie mfanye nini.
“Tunaweza kushauriana nao na tunashauriana nao kwa sababu sisi hatuna adui duniani, tuna uhusiano mzuri sana na Ulaya, tuna uhusiano mzuri na Marekani na tuna uhusiano mzuri na nchi zingine zote duaniani.
Akizungumzia ziara ya Rais Samia nchini Urusi, alisema imethibitisha mlengo wa Tanzania kutofungamana na upande wowote.
“Na juzi Rais wetu ameenda Urusi wengine wanauliza ameenda kufanya nini, mbona alivyoenda China hamkuuliza, mbona alipoenda Marekani hamkuuliza akienda Urusi mnaanza kuuliza ameenda kufanya nini.
“Ni mawazo yako kichwani ya kufikiri Marekani au Ulaya ya Magharibi ndio wenye dunia yao, lakini dunia ni ya wote.
“Sisi tangu mwasisi wetu Julius Nyerere alituambia ”katika dunia inayogombana sisi tusiwe na upande”, tukae katikati, wakigombana Warusi na Marekani sisi tunakaa katikati kwa hiyo ukienda Marekani baadae unaenda Urusi na wewe huna haja ya kuuliza tumeenda kufanya nini mbona hukuuliza tulipoenda Amerika (Marekani). Hatufungamani na upande wowote tunatazama hoja, tukiwa na hoja tunasema.
Alisema Chama kilijipa kazi ya kupambana na dhuluma ndani ya nchi na dhulma nje ya nchi, hivyo hakiwezi kuungana na dhulma “wala hatuwezi kulea dhulma ndani ya nchi, huo ndio uhuru tulio dai, ambaye haujui vizuri ndio huo kwa kuamua mambo yetu na kuhakikisha watu wetu wanaishi nabhawadhulumiwi.”
HAPI AWACHANA CHADEMA
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Ally Hapi, akizungumza katika mkutano huo, alisema madai ya CHADEMA kuwa wakipewa dola watafanya makubwa kwa wananchi hayana msingi, akidai kuwa walipopewa nafasi ya kuongoza majiji na manispaa mbalimbali nchini walishindwa kuleta maendeleo yaliyotarajiwa na badala yake walikumbwa na migogoro pamoja na hoja za ukaguzi zilizobainishwa katika ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Alisema viongozi wa CHADEMA wameendelea kutoa ahadi kubwa kwa wananchi wakati rekodi zao za uongozi katika maeneo waliyowahi kuongoza zinaonyesha tofauti.
“Hawa watu ni waongo, hawapaswi kuungwa mkono kwa namna yoyote ile. Tuwakatae kwa sababu wanachokisema hakilingani na matendo yao walipokuwa na nafasi za uongozi,” alisema Hapi.
Aidha, Hapi aliema CCM, kupitia vijana wa chama hicho, imejipanga kujibu hoja zote zinazotolewa na CHADEMA kwa kutumia takwimu na taarifa sahihi ili kuonyesha kile alichodai kuwa ni upotoshaji unaoenezwa na viongozi wa chama hicho kwa wananchi.


