Kauli ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo kwamba, “hatutachagua paka wa rangi gani, tutamtumia yeyote ilimradi anakamata panya,” imeibua tafsiri pana kuhusu mwelekeo wa Tanzania katika diplomasia ya kimataifa na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kauli hiyo inaashiria kuwa Tanzania haitachagua mshirika kwa misingi ya kisiasa au kiitikadi, bali itashirikiana na taifa lolote lenye uwezo wa kuchangia maendeleo ya taifa.

Katika kuelezea msimamo huo, Profesa Mkumbo alinukuu falsafa ya Rais wa kwanza wa Singapore, Lee Kuan Yew, aliyewahi kusema kuwa taifa halipaswi kujali “rangi ya paka,” bali uwezo wake wa “kukamata panya.”

Kwa tafsiri ya kisiasa na kiuchumi, kauli hiyo ina maana kuwa Tanzania ipo tayari kushirikiana na taifa lolote duniani ilimradi ushirikiano huo unaleta maendeleo, uwekezaji, teknolojia na manufaa kwa wananchi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na Rais Vladimir Putin wa Urusi. 

Profesa Mkumbo alitoa kauli hiyo Juni 7, 2026 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan nchini Urusi. Ziara hiyo ilivuta hisia za dunia kutokana na mapokezi makubwa aliyoyapata kutoka kwa Rais Vladimir Putin pamoja na uzito wa mazungumzo yaliyofanyika kati ya viongozi hao wawili.

Kauli hiyo inaakisi kwa uwazi sera ya Tanzania ya kutofungamana na upande wowote katika siasa za kimataifa. Katika dunia ya sasa yenye ushindani mkubwa wa kisiasa, kiuchumi na kiusalama kati ya mataifa makubwa kama Marekani, China na Urusi, Tanzania imeamua kuweka mbele maslahi ya taifa badala ya kufuata misimamo ya kambi za kimataifa.

Baba wa Taifa, Julius Nyerere. 

Sera hii ya kutofungamana si mpya katika historia ya Tanzania. Ni sehemu ya urithi wa diplomasia uliojengwa tangu enzi za Baba wa Taifa, Julius Nyerere. Hata hivyo, katika mazingira ya sasa ya dunia, sera hiyo imepewa sura mpya inayolenga zaidi diplomasia ya uchumi, uwekezaji, biashara, teknolojia na maendeleo ya wananchi.

Katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Tanzania inahitaji mtaji mkubwa, teknolojia za kisasa, miundombinu imara, nishati ya uhakika na soko la kimataifa.

Mahitaji hayo hayawezi kutimizwa kwa kutegemea taifa moja pekee au upande mmoja wa dunia. Ndiyo maana Tanzania imeamua kufungua milango kwa washirika mbalimbali bila kujali tofauti zao za kisiasa au kiitikadi.

  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kushoto na  Rais wa China Xi Jinping. 

Kwa mfano, Tanzania inaweza kushirikiana na China katika reli, viwanda na teknolojia; kushirikiana na Urusi katika sekta ya nishati, madini na elimu ya sayansi; huku ikiendelea kudumisha ushirikiano na mataifa ya Magharibi katika biashara, afya, utalii na uwekezaji.

Huu ndiyo msingi wa diplomasia ya kisasa inayoweka mbele matokeo badala ya mihemko ya kisiasa.
Faida kubwa ya sera hii ni kuiongezea Tanzania uhuru wa kuchagua fursa zenye manufaa zaidi kwa taifa. Nchi inapokuwa huru kushirikiana na kila upande, hupata nafasi kubwa ya kujadiliana kwa kujiamini, kuvutia wawekezaji wengi na kupata mikataba yenye ushindani na tija kwa wananchi wake.

Aidha, sera ya kutofungamana inaweza kuifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha biashara na diplomasia katika Afrika Mashariki. Mataifa mengi duniani yanatafuta nchi zenye utulivu wa kisiasa, sera rafiki za uwekezaji na mahusiano mazuri na pande zote za dunia.

Tanzania imeendelea kujijenga katika nafasi hiyo kutokana na utulivu wake wa kisiasa, jiografia yake ya kimkakati na uongozi unaolenga diplomasia ya uchumi.

Katika nyanja ya kisiasa, sera hii pia inalinda uhuru wa maamuzi ya taifa. Tanzania inaposhirikiana na kila upande bila kufungamana moja kwa moja na kambi yoyote ya kimataifa, huongeza uwezo wake wa kufanya maamuzi kwa kuzingatia maslahi yake yenyewe badala ya kushinikizwa na nguvu za mataifa makubwa.

Kiutamaduni, sera hii inafungua milango ya mwingiliano wa maarifa, elimu, utalii, sanaa na ubunifu kutoka sehemu mbalimbali duniani. Katika zama hizi za utandawazi, maendeleo hayategemei tena rasilimali pekee, bali pia uwezo wa taifa kujifunza kutoka kwa wengine huku likihifadhi utambulisho na maadili yake ya msingi.

Ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Urusi imeonesha namna Tanzania inavyozidi kujiamini katika diplomasia yake mpya ya kimataifa.

Mapokezi aliyoyapata kutoka kwa Rais Vladimir Putin yalionesha kuwa Tanzania sasa inaonekana kama mshirika muhimu katika siasa na uchumi wa dunia.

Hata hivyo, pamoja na kuimarisha ushirikiano na Urusi, Tanzania imeendelea kudumisha uhusiano mzuri na mataifa mengine ya Magharibi, Asia, Mashariki ya Kati na Afrika. Hii ndiyo tafsiri halisi ya sera ya kutofungamana na upande wowote — kuwa rafiki wa wote lakini mtumwa wa hakuna.

Katika muktadha wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kauli ya Profesa Kitila Mkumbo kuhusu “paka anayekamata panya” inaonesha kuwa Tanzania imeamua kuchagua ‘Pragmatizimu’ ya maendeleo badala ya siasa za makundi ya kimataifa. Taifa halitapima mshirika kwa itikadi yake, bali kwa mchango wake katika kuleta maendeleo, ajira, teknolojia, viwanda, uwekezaji na ustawi wa wananchi.

Mwisho wa siku, mataifa hayapimwi kwa upande wa kisiasa yanaouegemea, bali kwa kiwango cha maendeleo wanachowaletea wananchi wao. Tanzania inaonekana kuelekea katika njia mpya ya diplomasia ya maendeleo — njia inayotanguliza maslahi ya taifa, uchumi na ustawi wa wananchi wake.