*Ni zile zinazozalishwa katika Kiwanda cha Nguzo za Zege Mkoani Tabora

*Lengo ni kuboresha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme kwa wateja

Kampuni tanzu ya TANESCO ya kuzalisha nguzo za zege (TCPM) imeanza rasmi kusambaza nguzo za zege zinazozalishwa katika Kiwanda cha Nguzo za Zege kilichopo Mkoa wa Tabora, kwa lengo la kuimarisha na kuboresha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini.

Akizungumza Juni 4, 2026, wakati wa zoezi la upakiaji wa nguzo hizo kwa ajili ya kusambazwa katika maeneo mbalimbali nchini, hususani mkoa wa Tabora na mikoa jirani, Kaimu Meneja Mkuu wa TCPM, Mha. Khadija Abdallahmed, ameishukuru Serikali kupitia TANESCO kwa kuwezesha uanzishwaji wa kiwanda hicho, ambacho kinalenga kuimarisha miundombinu ya usambazaji wa umeme kwa wateja.

“Tunaishukuru sana Serikali kupitia TANESCO kwa kuwezesha kiwanda hiki. Leo tunashuhudia mafanikio makubwa baada ya kuanza kusambaza nguzo zilizozalishwa katika kiwanda chetu cha Tabora. Nguzo hizi sasa zinawafikia wateja wetu wa mkoa wa Tabora na mikoa jirani,” alisema Mha. Khadija.

Ameeleza kuwa nguzo za zege zinazozalishwa katika kiwanda hicho zina uwezo wa kudumu kwa kipindi cha miaka 50 hadi 100, zitasaidia kupunguza changamoto za kukatika kwa umeme zinazotokana na nguzo za miti kuoza, kuungua moto au kuanguka.

Kwa upande wake, Meneja wa Usanifu na Ubora wa TCPM, Mha. Emmanuel Mrema, amefafanua kuwa kiwanda hicho kimeleta maboresho makubwa katika usalama wa miundombinu ya umeme kwa kuzalisha nguzo zenye uwezo wa kuweka ‘’earth wire’’ ndani ya nguzo, tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

“Nguzo zetu zina ubora wa hali ya juu, hapo awali tulikuwa na changamoto ya uwekaji wa ‘’earth wire’’ kwa kuwa uliwekwa nje ya nguzo. Hali iliyochochea wizi wa waya huo na kuhatarisha usalama wa miundombinu ya TANESCO . Kupitia kiwanda hiki, sasa tunazalisha nguzo ambazo ‘’earth wire’’ huwekwa ndani ya nguzo ili kukabiliana na changamoto hiyo,” alisisitiza Mha. Mrema.

Kiwanda cha Kuzalisha Nguzo za Zege kinachosimamiwa na kampuni tanzu ya TANESCO, TCPM, kilijengwa mwaka 2024 na kukamilika Februari 2026 kwa gharama ya shilingi bilioni 7.9. Hadi sasa, kiwanda hicho kimezalisha nguzo 1,195 ambazo ziko tayari kusambazwa kwa wateja katika maeneo mbalimbali nchini.