Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Dk. Theresa Mugobi akizungumza kwrnye maonrsho hayo jijini Arusha leoMkurugenzi Mwenza wa Karibu-Kili Fair, Dominic Shoo akizungumza katika maonesho hayo jijini Arusha leo

Happy Lazaro,Arusha .

Arusha .Serikali imesema itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya utalii, kuboresha viwango vya malazi na huduma za ukarimu, kuharakisha matumizi ya teknolojia za kidijitali na kuimarisha ubora wa huduma ili kuongeza ushindani wa Tanzania katika soko la kimataifa la utalii.

Hayo yamesemwa jijini Arusha leo na Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Dk. Theresa Mugobi, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Ashatu Kijaji, wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Karibu-Kili Fair jijini Arusha.

Aidha maonesho ya Karibu Kilifair yameendelea kujidhihirisha kama moja ya matukio makubwa zaidi ya utalii katika Afrika Mashariki, yakikusanya pamoja waoneshaji, wanunuzi wa huduma za utalii, wawekezaji na wadau mbalimbali kutoka duniani kote kwa lengo kukuza biashara, uwekezaji na ushirikiano.

Dk. Mugobi amesema maonesho hayo yanaunga mkono jitihada za Serikali za kupanua masoko ya utalii na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika masoko ya jadi na yale yanayoibukia barani Afrika, Ulaya, Asia, Mashariki ya Kati na Amerika.

Amesema ushiriki wa zaidi ya waoneshaji 1,560 na wanunuzi wa huduma za utalii zaidi ya 500 kutoka nchi zaidi ya 40 unaonesha imani kubwa ambayo jumuiya ya kimataifa inaendelea kuwa nayo kwa Tanzania kama moja ya destinasheni bora za utalii na uwekezaji duniani.

“Sekta ya utalii inaendelea kuwa nguzo muhimu ya uchumi wa taifa kwa kuchangia takribani asilimia 17.2 ya Pato la Taifa na kutoa ajira zaidi ya milioni 2.5 za moja kwa moja zisizo za moja kwa moja kwa Watanzania,”amesema 

Dkt. Mugobi amesema Tanzania inaendelea kutumia mbinu mbalimbali za kisasa kuitangaza nchi, ikiwemo filamu ya “Tanzania: The African Dream”, ambayo imekuwa sehemu ya mkakati wa kuonesha uzuri wa vivutio vya Tanzania kwa hadhira ya kimataifa.

“Filamu hii inaonesha mchanganyiko wa kipekee wa vivutio vya Tanzania kuanzia wanyamapori, tamaduni, mandhari ya asili, fukwe, watu na urithi wa kihistoria. Tunaamini itawahamasisha mamilioni ya watu duniani kuichagua Tanzania kama destinasheni yao ya safari,” amesema.

Ameongeza kuwa Tanzania imebarikiwa kuwa na vivutio vya kipekee duniani ikiwemo Serengeti, Mlima Kilimanjaro, Ngorongoro, fukwe za Zanzibar pamoja na vivutio vya ukanda wa kusini na maeneo ya urithi wa utamaduni yanayovutia wageni kutoka sehemu mbalimbali za dunia.

“Tunao uhakika kuwa miaka bora zaidi ya utalii Tanzania bado ipo mbele yetu, na Visa imejipanga kuwa sehemu ya mafanikio hayo kwa kuhakikisha malipo ya kidijitali yanakuwa rahisi, salama na yanayopatikana kwa wote,” amesema.

Dkt. Mugobi amefafanua kuwa, Karibu Kilifair si maonesho ya kawaida bali ni uwekezaji wa kimkakati katika mustakabali wa utalii wa Tanzania, kwani mahusiano ya kibiashara yanayojengwa kupitia maonesho hayo yanachangia kuongeza watalii, kuvutia uwekezaji, kuzalisha ajira na kuboresha maisha ya wananchi.

Aidha, amesema Tanzania inaendelea kujiandaa kutumia kikamilifu fursa ya kuandaa Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027 kwa ushirikiano na Kenya na Uganda, huku Serikali ikiendelea kuwekeza katika miundombinu, teknolojia za kidijitali, ubora wa huduma na kampeni za masoko ili kuhakikisha sekta ya utalii inanufaika kikamilifu na tukio hilo la kihistoria.

“Sekta ya utalii inaendelea kuwa nguzo muhimu ya uchumi wa taifa kwa kuchangia takribani asilimia 17.2 ya Pato la Taifa na kutoa ajira zaidi ya milioni 2.5 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa Watanzania,” amesema Dkt. Mugobi.

Amebainisha kuwa chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, sekta ya utalii imepata mafanikio makubwa kutokana na uwekezaji wa Serikali katika miundombinu, uboreshaji wa huduma, utangazaji wa vivutio vya utalii na upanuzi wa masoko mapya ya utalii duniani.

Aidha ameongeza kuwa , mapato ya sekta hiyo yameongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 1.3 mwaka 2021 hadi zaidi ya dola bilioni 4.4 kwa sasa, hali inayodhihirisha ukuaji mkubwa wa sekta hiyo katika kipindi cha miaka michache iliyopita.

Naye Mkurugenzi Mwenza wa Karibu-Kili Fair, Dominic Shoo, amesema maonesho hayo yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kutangaza na kuuza bidhaa za utalii za Tanzania, huku akiiomba Serikali kuendelea kushirikiana na waandaaji wake ili kuongeza ufanisi wa sekta hiyo kuelekea matukio makubwa ikiwemo AFCON 2027.

Shoo amesema maonesho hayo yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kutangaza na kuuza bidhaa za utalii za Tanzania, huku akiiomba Serikali kuendelea kushirikiana na waandaaji wake ili kuongeza ufanisi wa sekta hiyo kuelekea matukio makubwa ikiwemo AFCON 2027.

Amesema mwaka huu maonesho hayo yamehusisha waoneshaji 550 kutoka Tanzania, Afrika Mashariki na mataifa mengine duniani ikilinganishwa na waoneshaji 500 wa mwaka.

Mwenyekiti wa Chama chama cha waongoza Watalii Tanzania (TATO), Willy Chambulo, amesisitiza umuhimu wa kuwashirikisha wafanyabiashara wadogo na wa kati katika maonesho ya utalii ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wananufaika na fursa za kiuchumi zinazotokana na sekta hiyo.

Amesema maonesho hayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kukuza biashara za utalii kwa kuwapa wafanyabiashara wa ngazi zote fursa ya kukutana moja kwa moja na wanunuzi kutoka mataifa mbalimbali.

Karibu Kilifair imekuwa sehemu muhimu ya kutangaza Tanzania na kuleta wanunuzi wa kimataifa. Hii inasaidia kukuza biashara na kuongeza idadi ya wageni wanaotembelea nchi yetu,” amesema Chambulo.

Ameongeza kuwa ushiriki mkubwa wa wanunuzi wa kimataifa unaonesha imani waliyonayo kwa Tanzania kama moja ya maeneo bora ya utalii duniani, huku akitabiri kuwa maonesho ya mwaka 2027 yatakuwa makubwa zaidi kutokana na ongezeko la washiriki na fursa za biashara.