Na Oscar Assenga,TANGA
SERIKALI imekipongeza Chama cha Washauri wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Tanzania (TACOGA) kwa kuendelea kuandaa mafunzo yanayolenga kuimarisha uwezo wa kitaaluma na kiutendaji wa washauri wa wanafunzi, wanasihi na viongozi wa serikali za wanafunzi kutoka vyuo mbalimbali nchini.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Tanga,Mkurugezi wa Maendeleo ya Jinsia kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalumu Badru Abdnur alisema mafunzo hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kuwajengea washiriki uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazowakabili wanafunzi katika taasisi za elimu ya juu.
Alisema katika kipindi cha mafunzo hayo, washiriki walipata nafasi ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujadili changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao, pamoja na kupata mbinu mpya zitakazowawezesha kuboresha huduma wanazozitoa kwa wanafunzi.
“Nawapongeza viongozi wa TACOGA kwa ubunifu na maono yao ya kuhakikisha mafunzo haya yanafanyika kila mwaka. Bila uongozi imara, kuandaa mafunzo ya aina hii si jambo rahisi,” alisema.
Aliongeza kuwa hatua hiyo inaonesha utambuzi wa umuhimu wa maendeleo endelevu ya kitaaluma kwa watendaji wanaohusika na huduma za wanafunzi pamoja na viongozi wa serikali za wanafunzi.
Badru alibainisha kuwa mada zilizowasilishwa zimegusa maeneo nyeti yanayoathiri ustawi na maendeleo ya wanafunzi, ikiwemo afya ya akili, maadili, matumizi ya teknolojia na uongozi bora.
Alisema dunia ya sasa inabadilika kwa kasi kutokana na maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kiteknolojia, hali inayowafanya vijana kuwa miongoni mwa makundi yanayoathirika zaidi na mabadiliko hayo.
“Vijana wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo afya ya akili, matumizi mabaya ya teknolojia, matumizi ya dawa za kulevya na mmomonyoko wa maadili. Hivyo, kuna haja ya kuendelea kuwajengea uwezo na kuwapa mwongozo sahihi ili wawe raia wema na wazalendo,” alisema.
Aidha, aliwakumbusha washiriki kuwa serikali na jamii kwa ujumla zinategemea sana mchango wa washauri na wanasihi katika kuwajenga wanafunzi.
Alisema wazazi na walezi wana matumaini makubwa kwa maafisa hao kwa kuwa vijana wengi wanaojiunga na vyuo vikuu bado wana umri mdogo na wanahitaji mwongozo, uangalizi na malezi ya karibu.
Kwa mujibu wake, kutokana na nafasi hiyo muhimu, TACOGA ina wajibu mkubwa wa kuchangia mageuzi ya maendeleo ya taifa kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Alitoa wito kwa chama hicho kuwekeza zaidi katika mifumo ya kiteknolojia ili kuendana na mazingira ya sasa ya kidijitali. Alisema ni muhimu kuanzisha mifumo ya kimtandao na programu za simu zitakazowezesha wanafunzi kupata huduma za ushauri kwa haraka na kwa urahisi bila kuathiri muda wao wa masomo.
Pia aliwataka kuendelea kujenga uwezo wa wanachama wao kupitia mafunzo endelevu ya saikolojia, unasihi na mbinu mpya za utoaji wa huduma ili kuwawezesha washauri na wanasihi kutoa suluhisho stahiki na la kisasa kwa changamoto zinazowakabili wanafunzi.
Vilevile, alisisitiza umuhimu wa kuimarisha viashiria vya kupima matokeo ya kazi zinazofanywa na TACOGA kwa kuwekeza katika tafiti ndogo ndogo za kutathmini kama huduma zinazotolewa zinaleta matokeo chanya katika ufaulu wa wanafunzi na maendeleo yao ya kijamii na kitaaluma.
Mgeni rasmi huyo pia alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya ofisi za washauri wa wanafunzi na madawati ya jinsia pamoja na vitengo vya kuzuia ukatili wa kijinsia katika vyuo vikuu. Alisema kuna muunganiko mkubwa wa majukumu kati ya taasisi hizo, hivyo ushirikiano ukiimarishwa utasaidia kupunguza mzigo wa kazi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wanafunzi.
Alisema maarifa na stadi zilizopatikana kupitia mafunzo hayo zinatarajiwa kuwafanya washiriki kuwa mabalozi wa mabadiliko katika taasisi zao na kuchangia kufikiwa kwa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TACOGA, Sophia Nchimbi, alisema chama hicho kimeendelea kuandaa mafunzo hayo kwa lengo la kuwawezesha maafisa wa ofisi za washauri wa wanafunzi katika vyuo vikuu kutekeleza majukumu yao kwa weledi zaidi.
Alisema washiriki walipata mafunzo yaliyohusu nidhamu chanya, usimamizi wa tabia, unasihi, matumizi salama ya mitandao ya kijamii, afya ya akili, malezi ya wanafunzi, uongozi bora na usimamizi wa madawati ya jinsia katika vyuo vikuu.
“Mafunzo haya yanatusaidia kupata ufumbuzi wa changamoto mbalimbali tunazokutana nazo katika maeneo yetu ya kazi. Maarifa tunayopata yanatupa uwezo wa kuwahudumia wanafunzi kwa ufanisi zaidi,” alisema Nchimbi.
Alisema mada kuhusu matumizi ya mitandao ya kijamii zimewawezesha washiriki kuelewa namna bora ya kuwaelekeza wanafunzi kutumia teknolojia kwa manufaa ya elimu badala ya matumizi yasiyofaa.
Nchimbi alisema pia washiriki walipata elimu kuhusu namna ya kusimamia madawati ya jinsia ili kuhakikisha wanafunzi wanaokumbana na changamoto mbalimbali wanapata msaada kwa wakati na kwa usahihi.
Aliongeza kuwa TACOGA imekuwa ikifanikiwa kuendesha mafunzo hayo kutokana na ushirikiano mkubwa wa wanachama na wadau mbalimbali wanaochangia maendeleo ya huduma za ushauri kwa wanafunzi.
Jumla ya washiriki 94 kutoka vyuo mbalimbali nchini walishiriki mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Tanga.
