NA DENIS MLOWE, IRINGA
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwigulu Nchemba, amewataka watumishi wa umma kote nchini kutoa huduma kwa wananchi kwa weledi, uadilifu na unyenyekevu, akisisitiza kuwa nafasi walizonazo ni za utumishi na si za kujionyesha mamlaka.
Akizungumza katika mkutano wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi wa Jimbo la Ismani mkoani Iringa, Dkt. Nchemba alisema serikali haitavumilia tabia ya baadhi ya watumishi wanaowazungusha wananchi kwa kuwapa usumbufu usio wa lazima wakati wa kutafuta huduma katika ofisi za umma.
Alisema wananchi wanaostahili kupata haki au huduma wanapaswa kuhudumiwa kwa wakati bila kucheleweshwa kwa sababu mambo ya urasimu usio na tija yamepitwa na wakati na yanachelewesha maendeleo ya wananchi pamoja na taifa kwa ujumla.
Waziri Mkuu alieleza kuwa watumishi wa umma wanapaswa kutambua kuwa mishahara yao inatokana na kodi zinazolipwa na wananchi, hivyo wanawajibika kuwahudumia kwa heshima na kujituma.
Alisema wananchi wengi hujinyima mahitaji mbalimbali ili kulipa kodi zinazowezesha serikali kujenga shule, vituo vya afya na miundombinu mingine muhimu pamoja na kugharamia mishahara ya watumishi.
Alionya dhidi ya tabia ya baadhi ya watumishi wanaopuuzia majukumu yao kwa kujishughulisha na simu au mazungumzo yasiyo ya kazi wakati wananchi wanahitaji huduma.
Alisema serikali iko tayari kuchukua hatua kali dhidi ya watumishi wasiowajibika, ikiwemo kuwafukuza kazi pale inapobainika kuwa wamekiuka maadili ya utumishi wa umma.
Dkt. Nchemba pia aliwataka wananchi kutokuwa waoga wanapofika katika ofisi za serikali kutafuta huduma, akisisitiza kuwa wana haki ya kuhudumiwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.
Aidha, alipendekeza watumishi wote wa umma wawe wanavaa vitambulisho vyenye majina yao kamili ili kurahisisha uwajibikaji na utambuzi wa wanaokiuka maadili ya kazi.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwahakikishia wananchi wa Ismani kuwa serikali itaendelea kutekeleza ahadi zote zilizotolewa wakati wa kampeni pamoja na zile zilizomo katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi.
Alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Ismani kwa juhudi zake za kufuatilia maendeleo ya jimbo hilo na kusukuma mbele agenda za wananchi katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu na miundombinu.
Alisema serikali itashirikiana kwa karibu na viongozi wa jimbo hilo kuhakikisha miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha ya wananchi inatekelezwa kwa wakati.
Dkt. Nchemba alisisitiza kuwa serikali itaendelea kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuhakikisha huduma bora zinapatikana na maisha ya Watanzania yanaendelea kuboreka.
Mwigulu alisisitiza kuwa dhamira ya serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, maendeleo na tabasamu waliloahidiwa kupitia utekelezaji wa miradi na mipango mbalimbali ya maendeleo inayolenga kuinua ustawi wa jamii na uchumi wa taifa.
Awali Mbunge wa Jimbo la Ismani,Emanuela Mtatifikolo Kaganda alimwomba Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba kusaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo hilo ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya, upatikanaji wa mashine ya X-Ray, mabweni ya wanafunzi wa kiume pamoja na kuharakisha mchakato wa kuanzishwa kwa Halmashauri ya Ismani.
Akizungumza katika mkutano huo luliofanyika katika Kata ya Kihologota wakati wa ziara ya Waziri Mkuu katika Jimbo la Ismani, Mtatifikolo alimshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kupeleka fedha za maendeleo zilizowezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali katika sekta za elimu, afya, maji, umeme na miundombinu.
Alisema wananchi wa Ismani wameendelea kunufaika na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita, huku akimpongeza Waziri Mkuu kwa usimamizi wake wa karibu katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa manufaa ya wananchi.
Mtatifikolo pia aliwashukuru wananchi wa Jimbo la Ismani kwa imani kubwa waliyoonyesha kwake katika uchaguzi, akiahidi kuitumia nafasi hiyo kuwatumikia kwa uadilifu na kujituma ili kutatua changamoto zinazowakabili.
Katika maombi yake kwa Waziri Mkuu, mbunge huyo alieleza kuwa Jimbo la Ismani bado lina upungufu wa vituo viwili vya afya katika kata za Nyang’oro na Izazi, hali inayowalazimu wananchi kusafiri umbali mrefu kupata huduma za afya. Alisema maeneo hayo yana changamoto za kijiografia ambazo zinafanya upatikanaji wa huduma kuwa mgumu zaidi, hivyo akaomba Serikali itoe fedha za ujenzi wa vituo hivyo.
Aidha, aliwasilisha ombi la wananchi la kutaka kuanzishwa kwa Halmashauri ya Ismani ili kusogeza huduma za utawala karibu zaidi na wananchi.
Alieleza kuwa baadhi ya wakazi hulazimika kutumia gharama kubwa za usafiri kufuata huduma za halmashauri kutokana na umbali mkubwa uliopo kati ya maeneo yao na makao ya halmashauri ya sasa.
Mbunge huyo pia aliomba Serikali kusaidia upatikanaji wa mashine ya X-Ray katika Kituo cha Afya cha Kihologota kinachohudumia kata kadhaa za eneo hilo,
Kwa upande wa elimu, Mtatifikolo alisema Serikali tayari imetoa fedha za ujenzi wa shule ya sekondari pamoja na mabweni ya wanafunzi wa kike, hivyo akaomba kuzingatiwa kwa ujenzi wa bweni la wanafunzi wa kiume ili kuhakikisha wanafunzi wote wanapata mazingira bora na salama ya kujifunzia.
Alisema utekelezaji wa maombi hayo utasaidia kuongeza upatikanaji wa huduma za kijamii na kuchochea maendeleo ya wananchi wa Jimbo la Ismani.