Na Beda Msimbe, TBN, St. Petersburg
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo anahitimisha ziara yake nchini Urusi kwa kushiriki katika Kongamano la Biashara kati ya Tanzania na Urusi sambamba na Jukwaa la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg (SPIEF 2026).
Katika kongamano hilo, Rais Samia anatarajiwa kuinadi Tanzania katika sekta mbalimbali za uwekezaji, biashara na ushirikiano wa kiuchumi ili kuvutia wawekezaji na kuongeza fursa za maendeleo kwa taifa.
Ziara ya Rais Samia nchini Urusi imeelezwa kuwa na mafanikio makubwa, hususan katika kuimarisha ushirikiano wa karibu kati ya Tanzania na Urusi katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu, maendeleo ya rasilimali watu na ukuzaji wa teknolojia.
Ziara hiyo katika taifa linalotajwa kuwa na nguvu kubwa katika teknolojia, uchakataji na uzalishaji wa viwandani pamoja na sekta ya kilimo, imefanyika wakati Tanzania ikijiandaa kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 yenye lengo la kulifanya taifa kufikia uchumi wa thamani ya dola trilioni moja kwa mwaka.
Kwa sasa, Serikali imesema uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika ambapo Pato la Taifa kwa mwaka 2025 lilikua kwa wastani wa asilimia 5.9 ikilinganishwa na asilimia 5.5 mwaka 2024.
Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Waziri wa Fedha, Balozi Dkt. Khamis Mussa Omar, wakati akiwasilisha Mapitio ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/2026 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni mjini Dodoma.
Balozi Omar alisema ukuaji huo umechangiwa na kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi, kuimarika kwa miundombinu ya usafiri na usafirishaji pamoja na kuongezeka kwa shughuli za kilimo.
Alitaja sababu nyingine kuwa ni kuongezeka kwa uzalishaji wa madini, shughuli za ujenzi wa umma na binafsi pamoja na utekelezaji wa miradi ya kimkakati, hususan katika sekta za nishati, usafirishaji na huduma za jamii.

