Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Leonard Akwilapo, ameliagiza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuendelea kusimamia kwa uthabiti ukusanyaji wa madeni yote halali ili kuimarisha uwezo wake wa kutoa huduma na kuendeleza uwekezaji katika sekta ya makazi nchini.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Bodi mpya ya Wakurugenzi ya NHC, Dkt. Akwilapo alisema Shirika halipaswi kuogopa kudai madeni ya wapangaji na wadaiwa wengine kwani malipo hayo ndiyo msingi wa uendelevu wa huduma zinazotolewa na Shirika.
“Msisite kudai madeni halali. Watu wanaoomba nyumba na huduma za NHC wanafahamu wajibu wao wa kulipa. Malipo hayo ndiyo yanayowezesha Shirika kuendelea kutoa huduma kwa wananchi wengine na kupanua uwekezaji wake,” alisema Waziri Akwilapo.
Alibainisha kuwa ukusanyaji mzuri wa mapato na madeni una mchango mkubwa katika kuimarisha hali ya kifedha ya Shirika, kuongeza uwezo wake wa kutekeleza miradi mipya na kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata huduma bora za makazi na biashara.
Waziri huyo pia aliipongeza Menejimenti ya NHC kwa mafanikio ya kifedha inayoendelea kuyapata, akieleza kuwa Shirika limeendelea kuwa miongoni mwa taasisi za umma zinazofanya vizuri na kutoa mchango muhimu kwa uchumi wa taifa.
