Serikali imewataka waajiri wote nchini kuhakikisha watumishi wa umma wanapewa mafunzo kuhusu usalama wa taarifa za Serikali na matumizi sahihi ya Akili Unde (AI), huku ikionya dhidi ya matumizi yanayokiuka maadili ya utumishi wa umma.
Akizungumza Juni 3, 2026 jijini Dodoma wakati wa kufunga kikao kazi cha Wakuu wa Idara za Utawala na Rasilimaliwatu katika sekta ya umma, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Ndege Qwaray, alisema Serikali imebaini changamoto za ukiukwaji wa maadili, matumizi ya lugha zisizofaa kwa wananchi pamoja na kutolindwa kwa taarifa za Serikali kupitia matumizi ya teknolojia.
Alisema watumishi wote wanapaswa kutumia barua pepe rasmi za Serikali katika mawasiliano ya kikazi ili kuimarisha usalama wa taarifa za Serikali. Aidha, alisisitiza kuwa hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi ya watumishi watakaobainika kutumia vibaya Akili Unde au mifumo rasmi ya mawasiliano ya Serikali.
Katika hatua nyingine, Serikali imetangaza kuwa itawachukulia hatua wasimamizi wa watumishi walioshindwa kutekeleza tathmini za utendaji kazi kwa wakati, hali iliyosababisha baadhi ya watumishi kukosa haki zao za kiutumishi ikiwemo kupandishwa vyeo.
Qwaray alisema baadhi ya wasimamizi hawakufanya tathmini za utendaji kwa mwaka 2024/2025, jambo lililoathiri maendeleo ya watumishi na kudhoofisha uwajibikaji katika utumishi wa umma. Kutokana na hali hiyo, amemuelekeza Katibu Mkuu (Utumishi) kwa kushirikiana na waajiri wote kuwabaini wasimamizi hao na kuwachukulia hatua stahiki, ikiwemo kuwaondoa katika nafasi za uongozi pale itakapobainika walishindwa kutekeleza majukumu yao bila sababu za msingi.
Ameongeza kuwa watumishi waliokosa sifa za kupandishwa vyeo kutokana na uzembe wa wasimamizi wao wanapaswa kupewa unafuu wa masharti ili wasikose haki zao za maendeleo ya kiutumishi.
Sambamba na hilo, Serikali imezitaka Idara za Utawala na Rasilimaliwatu katika taasisi za umma kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi ili kupunguza malalamiko ya watumishi na kuongeza imani ya wananchi kwa Serikali.
Qwaray alisema katika ziara zake amekutana na malalamiko mengi yanayohusu kutopandishwa vyeo kwa wakati, kuchelewa kulipwa stahili mbalimbali zikiwemo nauli za likizo na gharama za uhamisho. Alibainisha kuwa changamoto hizo kwa kiasi kikubwa zinasababishwa na kutokuzingatiwa kwa sheria, kanuni na miongozo inayosimamia utumishi wa umma.
Amevitaka vitengo vya Utawala na Rasilimaliwatu kuwa kiungo muhimu cha ushauri kwa viongozi na watumishi ili kuhakikisha haki za watumishi zinalindwa na huduma kwa wananchi zinaendelea kuboreshwa.

