Na John Bukuku, Dar es Salaam

Katika kipindi hiki ambacho Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya afya, Bohari ya Dawa (MSD) imeibuka kuwa moja ya taasisi zinazodhihirisha mabadiliko makubwa ya kimkakati ndani ya taasisi za umma.

Mafanikio hayo yanaonekana wazi kuwa ishara ya uimara wa afya ya taifa kwa siku za usoni kupitia mageuzi ya miundombinu ya kuhifadhi dawa na vifaa tiba yanayosimamiwa kwa umakini mkubwa na Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Bw. Mavere Tukai.

Kwa muda mrefu MSD ilikuwa ikikabiliwa na changamoto ya uhaba wa maghala ya kisasa ya kuhifadhi bidhaa za afya, hali iliyolazimu taasisi hiyo kukodi maghala kutoka sekta binafsi kwa gharama kubwa kila mwaka. Hata hivyo, ujio wa uongozi wa Tukai Mavere umeleta mwelekeo mpya wa kujenga uwezo wa ndani wa taasisi hiyo ili iweze kujitegemea kikamilifu katika uhifadhi na usambazaji wa dawa na vifaa tiba nchini.

Hatua kubwa iliyofikiwa kupitia ujenzi wa ghala la kisasa la Kanda ya Kati Dodoma ni ushahidi wa maono makubwa ya uongozi wa MSD. Ghala hilo lenye ukubwa wa mita za mraba 7,200 limekuwa kitovu muhimu cha uhifadhi wa bidhaa za afya katikati ya nchi na limeongeza uwezo wa taifa katika kuhakikisha upatikanaji wa dawa unakuwa wa uhakika zaidi.

Kukamilika kwa ghala hilo la Dodoma si mafanikio ya kawaida, bali ni hatua ya kimkakati inayolenga kuimarisha usalama wa dawa na vifaa tiba nchini. Kupitia miundombinu hiyo, MSD sasa ina uwezo mkubwa wa kuhifadhi bidhaa za afya katika mazingira yanayokidhi viwango vya kisasa vya kitaifa na kimataifa.

Mbali na kuongeza uwezo wa uhifadhi, ghala la Dodoma limekuwa msaada mkubwa katika kurahisisha usambazaji wa bidhaa za afya kwenda maeneo mbalimbali nchini kupitia miundombinu ya reli ya kisasa ya SGR na MGR. Hii imepunguza gharama za usafirishaji, kuongeza kasi ya huduma na kuimarisha ufanisi wa MSD katika kuwafikia wananchi kwa wakati.

Kinachovutia zaidi katika uongozi wa Bw. Tukai Mavere ni namna anavyofuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya taasisi yake. Ameonesha kuwa kiongozi mwenye maono, anayesimamia matumizi sahihi ya fedha za umma na kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa viwango vinavyokusudiwa.

Chini ya uongozi wake, MSD haijajikita tu katika kujenga maghala ya kawaida, bali imeelekeza nguvu katika ujenzi wa miundombinu yenye matumizi ya teknolojia za kisasa na nishati mbadala. Huu ni uthibitisho kuwa taasisi hiyo sasa inaangalia mustakabali wa muda mrefu wa sekta ya afya pamoja na suala la uhifadhi wa mazingira.

Ni kutokana na mtazamo huo ndipo MSD imeanza pia utekelezaji wa mradi mkubwa wa ujenzi wa ghala jipya la kisasa la Dar es Salaam lenye ukubwa wa mita za mraba 3,900 karibu na makao makuu ya sasa ya taasisi hiyo. Mradi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 12 na utaongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa uhifadhi wa bidhaa za afya nchini.

Faida kubwa ya mradi huo ni kwamba utawezesha MSD kuokoa zaidi ya Sh bilioni 2.3 kwa mwaka ambazo zimekuwa zikitumika kukodisha maghala binafsi. Huu ni mfano mzuri wa uongozi unaofikiria namna ya kupunguza gharama za uendeshaji huku ukiendelea kuboresha huduma kwa wananchi.

Kwa miaka mingi, taifa limekuwa likitumia fedha nyingi katika kukodi maghala kutokana na upungufu wa miundombinu ya kuhifadhia bidhaa za afya. Leo hii, kupitia mipango ya Tukai Mavere, MSD inaelekea kujenga mfumo imara wa kujitegemea ambao utaifanya taasisi hiyo kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kuhifadhi dawa na vifaa tiba kwa usalama na ufanisi.

Wakati huo huo, mipango mikubwa inayoendelea katika eneo la Kigamboni kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mingine ya MSD pamoja na makao makuu mapya ya taasisi hiyo, inaonesha wazi kuwa MSD sasa ipo katika hatua mpya ya maendeleo ya kimkakati. Uwekezaji huo utakuwa sehemu muhimu ya kuifanya taasisi hiyo kuwa ya kisasa zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Makao makuu mapya pamoja na maghala yatakayojengwa Kigamboni yanatarajiwa kuongeza uwezo mkubwa wa uhifadhi wa bidhaa za afya, kuimarisha mifumo ya usambazaji wa dawa na kuongeza ufanisi wa utoaji huduma kwa wananchi. Hii ni hatua muhimu katika kujenga usalama wa afya ya taifa kwa muda mrefu.

Jambo kubwa linalopaswa kupongezwa ni namna uongozi wa MSD chini ya Tukai Mavere ulivyoamua kuwekeza katika suluhisho la kudumu badala ya kutegemea njia za muda mfupi. Huu ni uamuzi wa kiuongozi unaoonesha uthubutu, weledi na uwezo wa kutazama mbele kwa maslahi mapana ya taifa.

Kwa hakika, mafanikio yanayoonekana leo ndani ya MSD yanatokana na usimamizi makini, ufuatiliaji wa karibu wa miradi na maamuzi yenye tija kwa taasisi na taifa kwa ujumla. Tukai Mavere ameonesha mfano wa kiongozi anayejali matokeo, anayesimamia maendeleo ya taasisi yake na mwenye dhamira ya kuifanya MSD kuwa imara zaidi.

Iwapo miradi yote inayoendelea ya Dodoma, Dar es Salaam na Kigamboni itakamilika kama ilivyopangwa, Tanzania itakuwa imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha usalama wa dawa na vifaa tiba kwa wananchi wake. Huu utakuwa msingi muhimu wa kuifanya nchi kuwa na mfumo wa kisasa, salama na wenye uhakika katika sekta ya afya kwa vizazi vya sasa na vijavyo.