Katika kipindi hiki ambacho Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya afya, Bohari ya Dawa (MSD) imeendelea kujidhihirisha kama moja ya taasisi za umma zinazotekeleza kwa vitendo mageuzi ya kimkakati yenye matokeo makubwa kwa taifa.

Mafanikio hayo yanaonekana wazi kupitia maboresho makubwa ya miundombinu ya kuhifadhi dawa na vifaa tiba yanayosimamiwa chini ya uongozi wa MSD kwa kushirikiana na Bodi ya Wakurugenzi ya taasisi hiyo.

Kwa muda mrefu, MSD ilikuwa ikikabiliwa na changamoto ya uhaba wa maghala ya kisasa ya kuhifadhi bidhaa za afya, hali iliyosababisha taasisi hiyo kutegemea maghala ya kukodi kutoka sekta binafsi kwa gharama kubwa kila mwaka.

Hata hivyo, kupitia maono ya uongozi wa MSD chini ya Bodi ya Wakurugenzi pamoja na usimamizi wa Mkurugenzi Mkuu Bw. Mavere Tukai na menejimenti yake, taasisi hiyo sasa imeanza kujenga mfumo imara wa kujitegemea katika uhifadhi na usambazaji wa dawa na vifaa tiba nchini. Hatua kubwa iliyofikiwa kupitia ujenzi wa ghala la kisasa la Kanda ya Kati Dodoma ni ushahidi wa dhamira ya kweli ya kuimarisha sekta ya afya nchini.

Ghala hilo lenye ukubwa wa mita za mraba 7,200 limeongeza uwezo wa taifa katika kuhifadhi bidhaa za afya kwa usalama na ufanisi mkubwa zaidi. Kukamilika kwa ghala hilo la Dodoma si mafanikio ya kawaida, bali ni hatua ya kimkakati inayolenga kuijengea Tanzania uwezo wa muda mrefu wa kuhifadhi dawa na vifaa tiba katika mazingira yanayokidhi viwango vya kisasa vya kitaifa na kimataifa.

Mbali na kuongeza uwezo wa uhifadhi wa bidhaa za afya, ghala hilo limekuwa msaada mkubwa katika kurahisisha usambazaji wa dawa kwenda maeneo mbalimbali ya nchi kupitia matumizi ya reli za kisasa za SGR na MGR. Hii imepunguza gharama za usafirishaji na kuongeza kasi ya utoaji wa huduma kwa wananchi.

Kinachopaswa kupongezwa zaidi ni namna uongozi wa MSD chini ya Bodi ya Wakurugenzi ulivyojikita katika uwekezaji wa muda mrefu badala ya kutegemea suluhisho za muda mfupi. Huu ni mfano wa taasisi inayofikiria mustakabali wa taifa katika eneo nyeti la afya.

Kupitia usimamizi wa Bodi ya wakurugenzi Mkurugenzi Mkuu Bw. Mavere Tukai na menejimenti yake , MSD imeonesha uwezo mkubwa wa kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi yake, kuhakikisha matumizi sahihi ya fedha za umma pamoja na kusimamia miradi hiyo kwa viwango vinavyokusudiwa.

Chini ya uongozi huo, MSD haijajikita tu katika kujenga maghala ya kawaida, bali imeelekeza nguvu katika matumizi ya teknolojia za kisasa pamoja na nishati mbadala ili kuongeza ufanisi wa matumizi ya nishati, kupunguza gharama za uendeshaji na kuunga mkono jitihada za uhifadhi wa mazingira.

Ni katika mwelekeo huo ndipo MSD imeanza utekelezaji wa mradi mkubwa wa ujenzi wa ghala jipya la kisasa la Dar es Salaam lenye ukubwa wa mita za mraba 3,900 karibu na makao makuu ya sasa ya taasisi hiyo.

Mradi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 12 na utaongeza uwezo mkubwa wa uhifadhi wa bidhaa za afya nchini. Faida kubwa ya mradi huo ni kwamba utawezesha MSD kuokoa zaidi ya Sh bilioni 2.3 kwa mwaka ambazo zimekuwa zikitumika kukodisha maghala binafsi. Huu ni ushahidi kuwa uongozi wa taasisi hiyo unaweka mbele matumizi yenye tija ya fedha za umma huku ukiendelea kuboresha huduma kwa wananchi.

Kwa miaka mingi taifa limekuwa likikabiliwa na changamoto ya upungufu wa miundombinu ya kisasa ya kuhifadhi dawa na vifaa tiba. Leo hii, kupitia mipango ya MSD chini ya Bodi ya Wakurugenzi na usimamizi wa Mkurugenzi Mkuu Bw. Mavere Tukai na menejimenti yake , taasisi hiyo inaelekea kujenga mfumo wa kisasa utakaoiwezesha kujitegemea kikamilifu katika uhifadhi wa bidhaa za afya.

Wakati huo huo, mipango mikubwa inayoendelea katika eneo la Kigamboni kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mingine ya MSD pamoja na makao makuu mapya ya taasisi hiyo, inaonesha wazi kuwa MSD sasa ipo katika hatua mpya ya maendeleo ya kimkakati. Makao makuu hayo pamoja na maghala yatakayojengwa Kigamboni yanatarajiwa kuongeza uwezo mkubwa wa taifa katika kuhifadhi dawa na vifaa tiba, kuimarisha mifumo ya usambazaji wa bidhaa za afya na kuongeza ufanisi wa huduma kwa wananchi.

Kwa hakika, mafanikio yanayoonekana leo ndani ya MSD yanatokana na usimamizi makini wa uongozi wa taasisi hiyo chini ya Bodi ya Wakurugenzi, pamoja na ufuatiliaji wa karibu wa utekelezaji wa miradi mbalimbali unaofanywa na Mkurugenzi Mkuu Bw. Mavere Tukai na timu yake. Iwapo miradi yote ya Dodoma, Dar es Salaam na Kigamboni itakamilika kama ilivyopangwa, Tanzania itakuwa imepiga hatua kubwa katika kuhakikisha usalama wa dawa na vifaa tiba kwa wananchi wake.

Huu utakuwa msingi muhimu wa kuifanya nchi kuwa na mfumo wa kisasa, salama na wenye uhakika wa huduma za afya kwa vizazi vya sasa na vijavyo.