Na. SSGT Mawazo Mtondo – DODOMA 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. John Jingu, amepongeza ushirikiano imara uliopo kati ya Wizara ya Katiba na Sheria na Jeshi la Magereza katika kuimarisha upatikanaji wa haki na huduma za msaada wa kisheria kwa Wafungwa na mahabusu kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za nchi.

Dkt. Jingu amesema kuwa, Wizara ya Katiba na Sheria itaendelea kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Magereza katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kuwajengea uwezo wataalamu wa sheria, kuimarisha utekelezaji wa vifungo mbadala, utoaji haki pamoja na kuboresha mifumo ya ukusanyaji, uchambuzi na uwasilishaji wa taarifa zinazohusu huduma za msaada wa kisheria na ufuatiliaji wa haki za wafungwa na mahabusu.

Amesisitiza kuwa, lengo la Serikali ni kuhakikisha Magereza yanabaki kuhifadhi wale tu wanaostahili kuwepo kwa mujibu wa sheria, na kutumia ipasavyo fursa nyingine za kisheria kwa wanufaika wanaostahili ili kupunguza msongamano magerezani.

Dkt. Jingu alitoa kauli hiyo leo Juni 3, 2026, katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Katiba na Sheria uliopo Mtumba, Jijini Dodoma, wakati wa kikao cha pamoja kati ya viongozi wa Wizara hiyo na Jeshi la Magereza kilicholenga kujadili na kuimarisha ushirikiano katika masuala ya utoaji haki na huduma za msaada wa kisheria magerezani.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Jeshi la Magereza, CGP Jeremiah Yoram Katungu, amesema ushirikiano kati ya Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Jeshi la Magereza ni nguzo muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya taasisi hizo na kufikia malengo ya Serikali ya kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wananchi.

Ameeleza kuwa, maeneo ya ushirikiano yanajumuisha utoaji wa mafunzo kwa maafisa wa sheria, uimarishaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa wafungwa na mahabusu, pamoja na kushughulikia changamoto mbalimbali za kisheria zinazowakabili watu waliopo magerezani.

CGP Katungu amesema kuwa, Jeshi la Magereza linaendelea kutekeleza kwa mafanikio mfumo wa Mahakama Mtandao unaowezesha baadhi ya mashauri kusikilizwa kwa wafungwa na mahabusu wakiwa ndani ya magereza, hatua inayochangia kupunguza gharama za uendeshaji wa magereza, kuongeza ufanisi na kupunguza changamoto za usafirishaji wa wafungwa kwenda na kutoka mahakamani.

Amesema hadi sasa magereza 84 nchini tayari yameunganishwa na mfumo huo, huku Wizara ya Katiba na Sheria ikiwa imechangia vifaa vya TEHAMA katika vituo 30, jambo ambalo limeongeza ufanisi katika usikilizwaji wa mashauri na kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wakati.

Aidha, CGP. Katungu ameeleza kuwa kwa mujibu wa Kifungu cha 36 cha Sheria ya Msaada wa Kisheria, Sura ya 21, pamoja na Kanuni ya 23 na 27 za Kanuni za Msaada wa Kisheria za mwaka 2018, Jeshi la Magereza lina wajibu wa kuwezesha upatikanaji wa huduma za msaada wa kisheria kwa wafungwa na mahabusu waliopo magerezani.

Ameongeza kuwa Jeshi la Magereza lina wataalamu wa sheria katika magereza yote 129 nchini, Ofisi zote za Magereza za Mikoa pamoja na Makao Makuu ya Jeshi, ambapo Divisheni ya Sheria na Uendeshaji wa Magereza inaratibu masuala yote ya kisheria. Vilevile, madawati ya msaada wa kisheria yameimarishwa katika magereza mbalimbali nchini ili kuhakikisha wafungwa na mahabusu wanapata huduma za msaada wa kisheria kwa wakati, kwa ufanisi na kwa kuzingatia misingi ya haki na utawala wa sheria.

Kikao hicho ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuendelea kuimarisha mfumo wa haki jinai nchini na kuhakikisha taasisi zote zinazohusika na utoaji wa haki zinashirikiana kwa karibu katika kutekeleza majukumu yao kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.