Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) zimeahidi kuimarisha zaidi ushirikiano katika sekta mbalimbali za kiuchumi ikiwemo biashara na uwekezaji.
Hayo yameelezwa wakati wa mkutano kati ya Waziri wa Fedha, wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), na Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) nchini Tanzania, Mhe. Khalifa Abdulrahman Al Marzouqi, uliofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam.
Mhe. Balozi Omar, aliishukuru Serikali ya UAE kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za maendeleo ya Tanzania kupitia ushirikiano katika sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi na kusisitiza dhamira ya Serikali ya Tanzania ya kuendelea kuimarisha ushirikiano huo katika maeneo ya biashara, uwekezaji, miundombinu, nishati na teknolojia.
Naye Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) nchini Tanzania, Mhe. Khalifa Abdulrahman Al Marzouqi, alieleza kuridhishwa na ushirikiano mzuri uliopo kati ya nchi hizo mbili na kuahidi kuendelea kuhamasisha wawekezaji kutoka UAE kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali za kipaumbele kwa maendeleo ya uchumi wa Taifa kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania na UAE.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Kaimu Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha ambaye pia ni Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje, Bw. Rished Bade, Mchumi kutoka Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Jabir Selemani, Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Lawrence Gwape na Afisa wa Idara ya Mashariki ya Kati kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Shamim Khalfan.

