Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akisalimiana na Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi, na viongozi mbalimbali alipowasili katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ajili ya kuhudhuria Kongamano la Vijana, linalofanyika Jijini Dar es Salaam, Juni 2, 2026, ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo kilele chake ni Juni 5, 2026.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akikagua mabanda ya maonesho mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam linapofanyika Kongamano la Vijana kuhusu mazingira, linalofanyika Jijini Dar es Salaam, Juni 2, 2026 ambayo ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambapo kilele chake ni Juni 5, 2026.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni akipanda mti eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mara baada ya kuwasili katika viwanja vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam linapofanyika Kongamano la Vijana kuhusu mazingira, linalofanyika Jijini Dar es Salaam, Juni 2, 2026.
…………..
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yusuf Masauni, ameiagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pamoja na Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) kuongeza bajeti kwa ajili ya programu za vijana wa kujitolea ili kuwajengea uzoefu wa kazi na kuwaandaa kwa ajira za baadaye.
Mhandisi Masauni alisema hatua hiyo itasaidia taasisi hizo kunufaika na ubunifu, maarifa mapya na uwezo wa vijana katika matumizi ya teknolojia, huku ikitoa fursa kwa wahitimu kupata uzoefu wa moja kwa moja katika masuala ya mazingira, mabadiliko ya tabianchi na usimamizi wa kaboni.
Alisema vijana wanaopata nafasi za kujitolea wanapaswa kushirikishwa kikamilifu katika utekelezaji wa shughuli za kitaalamu na maendeleo ya mifumo ya kidijitali ili kuongeza ufanisi wa taasisi na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Ni muhimu NEMC na NCMC kutenga rasilimali za kutosha kwa ajili ya vijana wa kujitolea kwa sababu hawa ndiyo wataalamu wa kesho. Kupitia programu hizi wanapata uzoefu wa vitendo unaowaandaa kwa ajira na kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi,” alisema Masauni.
Alifafanua kuwa programu za kujitolea zina manufaa kwa pande zote mbili, kwani vijana hupata uzoefu unaohitajika katika soko la ajira, huku taasisi zikipata fursa ya kuwafahamu kwa karibu uwezo wao wa kazi, nidhamu, ubunifu na uwezo wa kutatua changamoto mbalimbali.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, inapojitokeza nafasi za ajira taasisi zinakuwa katika nafasi nzuri ya kupata watumishi wenye uwezo na uzoefu kwa kuwa tayari wamefanya kazi nao kupitia programu za kujitolea na kuthibitisha uwezo wao katika mazingira halisi ya kazi.
Aidha, alisema ushiriki wa vijana katika miradi ya mazingira na ufuatiliaji wa kaboni unaweza kusaidia kuibua suluhisho za kisasa zinazotumia teknolojia katika ukusanyaji, uchambuzi na usimamizi wa taarifa muhimu za mazingira kwa ajili ya kufanya maamuzi sahihi.
Mhandisi Masauni alisisitiza kuwa uwekezaji kwa vijana ni uwekezaji wa moja kwa moja katika maendeleo ya taifa, akizitaka taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais kuendelea kubuni na kuimarisha mifumo itakayoongeza ushiriki wa vijana katika shughuli za maendeleo na uhifadhi wa mazingira nchini.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi, alisema kuwa kuwajengea uwezo vijana kupitia programu za kujitolea ni mkakati muhimu wa kuandaa kizazi kitakachosimamia agenda za maendeleo endelevu, uhifadhi wa mazingira na uchumi wa kijani.
Alisema Afrika ina hazina kubwa ya rasilimali watu, ambapo takribani asilimia 40 ya vijana wa dunia wanaishi katika bara hilo, jambo linalotoa fursa kubwa ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kiteknolojia endapo vijana hao watapatiwa elimu, ujuzi na nafasi za kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Dkt. Muyungi alisema programu za kujitolea zinawawezesha vijana kupata uzoefu wa kazi unaohitajika katika soko la ajira, huku zikizisaidia taasisi kupata kundi la vijana wenye maarifa, ubunifu na uwezo wa kutumia teknolojia katika kutatua changamoto mbalimbali za maendeleo.
Aliongeza kuwa vijana wana mchango mkubwa katika kuibua mawazo mapya na suluhisho za kisasa zinazoweza kusaidia kukabiliana na changamoto za mazingira na mabadiliko ya tabianchi, hivyo ni muhimu kuendelea kuwekeza katika kuwawezesha kushiriki katika miradi na programu mbalimbali za kitaifa.
“Tunapowapa vijana fursa za kujifunza, kufanya kazi na kushiriki katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi zetu, tunakuwa tunaandaa msingi imara wa kupata wataalamu na viongozi bora wa baadaye watakaosukuma mbele maendeleo ya Tanzania, Afrika na dunia kwa ujumla,” alisema Dkt. Muyungi.
