NA FAUZIA MUSSA

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Fedha na Mipango imetiliana saini mikataba miwili ya ujenzi na kampuni ya Stabit Corporation Limited pamoja na Salem Construction Limited chini ya Mradi wa BIG-Z, unaolenga kuimarisha miundombinu ya mijini, usimamizi wa mazingira na huduma za kijamii Zanzibar.

Mikataba hiyo inahusisha ujenzi wa Kituo cha Kukusanyia Taka cha Fuoni Chunga (Solid Waste Transfer Station) pamoja na utekelezaji wa Mradi Salama wa Watembea kwa Miguu katika maeneo ya Mji Mkongwe (Stone Town Safe and Sustainable Mobility Program).

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Aboud Hussein Mwinyi, alisema kusainiwa kwa mikataba hiyo ni hatua muhimu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayolenga kuimarisha maisha ya wananchi pamoja na mazingira ya miji.

Alisisitiza umuhimu wa wakandarasi kuzingatia ubora wa kazi, kusimamia muda wa utekelezaji kwa ufanisi na kuhakikisha kunakuwa na uratibu mzuri katika kipindi chote cha ujenzi.

“Tunatarajia kuona kazi zenye viwango bora, utekelezaji unaokwenda sambamba na muda uliopangwa pamoja na ushirikiano mzuri na jamii inayozunguka maeneo ya miradi,” alisema.

Aidha, aliwataka wakandarasi kuwa na mipango kazi madhubuti itakayosaidia utekelezaji wa miradi hiyo kufanyika bila kusababisha usumbufu kwa wananchi, wafanyabiashara na shughuli nyingine za kijamii katika maeneo husika.

“Kukamilika kwa miradi hii kutaimarisha miundombinu ya mijini, usimamizi wa taka ngumu pamoja na kuweka mazingira salama na rafiki kwa watembea kwa miguu, hususan katika eneo la Mji Mkongwe ambalo ni kitovu cha urithi wa kihistoria na shughuli za kijamii na kiuchumi Zanzibar,” alisema Mwinyi.

Kwa upande wao, wakandarasi waliopewa zabuni hizo walieleza utayari wao wa kutekeleza masharti yote yaliyowekwa katika mikataba hiyo, huku wakiahidi kuzingatia viwango vya ubora, usalama wa wafanyakazi, uhifadhi wa mazingira na maslahi ya jamii inayozunguka maeneo ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Abuzer Salem kutoka kampuni ya Salem Construction Limited alisisitiza dhamira yao ya kuhakikisha shughuli za ujenzi zinafanyika kwa weledi na kwa namna itakayopunguza athari kwa wakazi wa maeneo husika.

Mradi wa ujenzi wa Kituo cha Kukusanyia Taka Fuoni Chunga pamoja na Mradi Salama wa Watembea kwa Miguu Mji Mkongwe ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi Mkubwa wa BIG-Z unaosimamiwa na Wizara ya Fedha na Mipango, ukiwa na lengo la kuendeleza miundombinu endelevu na kuboresha mazingira ya maisha ya wananchi wa Zanzibar.