Na Hassan Kimweri, WAF – Dar es Salaam

Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe amesema Serikali itaendelea kuhakikisha kila mama na mtoto mchanga wanapata huduma bora, salama na zenye viwango kupitia uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya nchini na kufikia malengo ya Kimataifa. 

Dkt. Magembe amesema hayo leo Mei 28, 2026 katika hafla fupi iliyofanyika katika hospitali ya Mwananyamala Jijini Dar es Salaam ya kupokea na kukabidhi vifaa tiba ikiwemo magari mawili yatakayosaidia huduma za mama na mtoto nchini. 

“Serikali imeendelea kuimarisha mazingira ya kazi kwa wahudumu wa afya pamoja na kuongeza uwezo wa wakunga ili kuhakikisha huduma za afya ya uzazi na mtoto zinawafikia wananchi kwa ubora unaotakiwa,” amesema Dkt. Magembe 

Aidha, Dkt. Magembe amesema kuwa ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo umeendelea kuleta matokeo chanya katika sekta ya afya, hususan katika kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto.

Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka ubalozi wa Canada nchini Tanzania Mhe. Kevin Tokar amefurahishwa na utekelezaji wa mradi huo na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuiamarisha huduma za ukunga nchini kwa kuwa huduma hizo zina mchango mkubwa wa kuokoa maisha ya mama na mtoto.  

Nae, Mwakilishi wa UNFPA Tanzania Bw. Mark Bryan Schreiner amesema uwekezaji katika wakunga ni hatua muhimu ya kuhakikisha ujauzito salama na maisha bora kwa wanawake pamoja na watoto wachanga.

Pia, Mkunga Elizabeth Kawogo kutoka moja ya vituo vya afya vilivyonufaika na mradi huo amesema vifaa vya ‘Learning Corner’ vimeleta mabadiliko makubwa katika namna wanavyojifunza na kutoa huduma kwa kina mama na watoto.

Mradi wa Thamini Uzazi Salama (SMIT) ni mradi wa miaka saba unaotekelezwa na UNFPA kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kwa ufadhili wa Global Affairs Canada, ukiwa na lengo la kuongeza idadi ya wakunga wenye ujuzi na kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto katika mikoa ya Dar es Salaam na Shinyanga.