Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Bw. Balandya Elikana amesema ajenda ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira ni eneo la kipaumbele katika mipango ya maendeleo ya mkoa huo.
Bw. Elikana amesema hayo leo Mei 29, 2026 wakati wa mazungumzo baina na timu ya watalaamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais waliofika ofisini kwake kwa ajili ya kupokea taarifa ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku Mazingira Duniani, 2026 katika Mkoa huo.
Elikana amesema Mkoa huo umekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha juhudi za Serikali katika masuala ya utunzaji na usimamizi wa mazingira kwa kuhimiza jamii umuhimu wa za uhifadhi wa mazingira ikiwemo upandaji miti na shughuli za usafi.
Ameeleza kuwa kwa kuzingatia umuhimu wa mazingira, Sekretarieti ya Mkoa huo kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya zipo mbioni kuandaa utaratibu wa kuhamasisha vijana kuweza kushiriki katika utunzaji na uhifadhi wa misitu katika maeneo mbalimbali Mkoani humo.
“Mwanza tuna misitu mingi mfano msitu wa buhindi uliopo halmashauri ya buchosa ambao kwa sasa tunataka maeneo ya aina hii yaweze kutumika vyema kuwanufaisha vijana kwani ni fursa inayoweza kutengeneza ajira” amesema Elikana.
Aidha amesema hivi karibuni Mkoa huo ulikuwa mwenyeji wa Maadhimisho ya Siku ya Ziwa Victoria yaliyolenga kuhimiza jamii kuhusu umuhimu wa utunzaji na uhifadhi wa mazingira katika ziwa hilo ambalo lina mchango mkuwa katika shughuli za kijamii na kiuchumi.
“Maadhimisho haya ni sehemu ya utekelezaji wa azimio la Jumuiya ya Afrika Mashariki kupitia kamisheni ya bonde la ziwa Victoria…..tulikuwa na matukio mbalimbali ikiwemo zoezi la upandaji wa miti takribani 2500 katika eneo la mradi wa maji Butimba” amesema Elikana.
Kwa upande kiongozi wa timu ya wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Afisa Misitu Mwandamizi Bw. Lucas Sabida ameupongeza Mkoa wa Mwanza kwa juhudi mbalimbali inazoendelea kuzifanya katika kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa uhifadhi na utunzaji wa mazingira.
Aidha amesema Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kupata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa timu ya wataalamu wa Mazingira ya Mkoa huo na kuufanya kuwa ni miongoni mwa Mkoa ya mfano katika uhamasishaji wa jamii kuhusu umuhimu wa kutunza na kuhifadhi wa mazingira.
Timu ya Wataalamu ya Ofisi ya Makamu wa Rais ipo Mkoani Mwanza kwa ajili ya kuratibu maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani Mkoani humo yatayoadhimishwa kimkoa siku ya Jumamosi tarehe 30 Mei, 2026.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo anatarajia kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda. Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani mwaka 2026 yamebeba kauli mbiu isemayo “Dira 2050: Tuwajibike Kukijanisha Tanzania”.

