
Naibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Ilala, Moza Kasubi akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 28, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa TAKUKURU kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2026.
…………
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Ilala imefanikiwa kuokoa shilingi milioni 57.5 kupitia kesi ya uhujumu uchumi namba 2458 ya mwaka 2024 iliyowahusisha washtakiwa wanne waliokuwa wakikabiliwa na makosa ya ubadhirifu, ufujaji wa mali za umma pamoja na matumizi mabaya ya madaraka.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 28, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa TAKUKURU kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2026, Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Ilala, Moza Kasubi, amesema washtakiwa hao waliisababishia hasara Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) kwa kufanya ubadhirifu wa shilingi milioni 115.
Amesema kuwa kati ya fedha hizo, kiasi cha shilingi milioni 57 kilirejeshwa katika akaunti ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) iliyopo Benki Kuu ya Tanzania.
Kasubi amesema kuwa katika kipindi hicho TAKUKURU Ilala ilipokea jumla ya malalamiko 27, ambapo malalamiko 26 yalihusu vitendo vya rushwa na yanaendelea kufanyiwa uchunguzi, huku shauri moja likibainika kutohusiana na rushwa na mhusika kushauriwa kufika katika mamlaka husika.
Katika hatua nyingine, TAKUKURU Ilala imefuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 52.08.
Miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa Kituo cha Polisi Bonyokwa wenye thamani ya shilingi milioni 406.6, ambao ulikwama kutokana na mkandarasi kutolipwa kwa wakati.
Kasubi amesema kuwa mkandarasi wa mradi huo, Kampuni ya M/s Nyakire Investment Limited, alikuwa amesitisha ujenzi kabla ya TAKUKURU kuingilia kati.
Kufuatia ufuatiliaji huo, mkandarasi huyo alilipwa shilingi milioni 181.9 alizokuwa anadai Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kazi zilizotekelezwa.
Pia amesema TAKUKURU imeendelea kufuatilia matumizi ya fedha katika miradi mbalimbali ya maendeleo na kuhakikisha kasoro zilizobainika zinarekebishwa ili miradi itekelezwe kwa kuzingatia thamani ya fedha iliyotengwa.
Miradi iliyofuatiliwa ni pamoja na ujenzi wa Kitega Uchumi cha DCC Kariakoo wenye thamani ya shilingi bilioni 36.7, ujenzi wa barabara ya Lindi kwa kiwango cha lami wenye thamani ya shilingi bilioni 2.84, ujenzi wa kisima cha maji Mchikichini wenye thamani ya shilingi milioni 164, pamoja na ujenzi wa Kituo cha Afya Mchikichini wenye thamani ya shilingi bilioni 7.7.
Miradi mingine ni ujenzi wa Shule ya Sekondari Kitunda Relini wenye thamani ya shilingi bilioni 4.2, pamoja na ufuatiliaji wa mkopo wa shilingi milioni 40 uliotolewa kwa kikundi cha vijana cha Fighters cha Segerea kinachojishughulisha na usafirishaji wa abiria kwa kutumia bodaboda kupitia mpango wa mikopo ya Halmashauri kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Kwa upande wa elimu kwa umma, TAKUKURU Ilala imefanikiwa kuwafikia wananchi zaidi ya 19,320 kupitia semina, vipindi vya redio na televisheni pamoja na njia nyingine za utoaji elimu kuhusu mapambano dhidi ya rushwa.
Pia klabu 33 za wapinga rushwa zimeimarishwa kupitia utoaji wa mada mbalimbali kuhusu athari za rushwa. Pia semina 28 zilitolewa kwa watumishi wa umma sambamba na vipindi vinne vya redio na televisheni vilivyolenga kuongeza uelewa kuhusu madhara ya rushwa na umuhimu wa uwajibikaji kwa uadilifu.
TAKUKURU Mkoa wa Ilala imetoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na taasisi hiyo katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi na huduma bora zinapatikana kwa jamii, huku kila mwananchi akishiriki katika mapambano dhidi ya rushwa.
