………..

Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeendelea kuonesha dhamira ya kuimarisha sekta ya makazi na biashara nchini kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), huku miradi kadhaa ya kimkakati ikitarajiwa kukamilika ndani ya mwaka 2026 na mingine kuanza rasmi mwaka wa fedha 2026/27.

Akiwasilisha Bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka 2026/27, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo amesema Serikali kupitia NHC imeendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya nyumba, biashara na uwekezaji inayolenga kuongeza upatikanaji wa makazi bora pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi wa miji mbalimbali nchini.

Katika hotuba hiyo, Mhe. Dkt. Akwilapo amesema ujenzi wa nyumba 422 katika mradi wa Kawe 711 jijini Dar es Salaam wenye thamani ya shilingi bilioni 169 umefikia asilimia 85 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika ifikapo Juni 30, 2026. Aidha, mradi wa nyumba 196 wa Golden Premier Residence (GPR) wenye thamani ya shilingi bilioni 127 umefikia asilimia 50 huku ukitarajiwa kukamilika mwaka 2027.

Waziri huyo amesema Serikali pia inaendelea na maandalizi ya utekelezaji wa miradi mipya ya makazi kupitia mpango wa nyumba 5,000 wa Samia Housing Scheme katika maeneo ya Mtoni Kijichi na Kawe jijini Dar es Salaam pamoja na Medeli na Iyumbu jijini Dodoma.

“Katika mwaka 2026/27, Shirika litaendelea na ujenzi wa nyumba katika miradi ya Samia Housing Scheme sambamba na kuanza utekelezaji wa miradi mipya katika maeneo ya Njedengwa Dodoma, Urafiki Dar es Salaam, Makongoro Mwanza na Sokoine Complex Arusha,” amesema Mhe. Dkt. Akwilapo.

Kwa upande wa nyumba za gharama nafuu, Waziri Akwilapo amesema NHC limekamilisha maandalizi ya awamu ya kwanza ya ujenzi wa nyumba 800 katika maeneo ya Salama Creek Kigamboni, Sabasaba Morogoro, Iyumbu Dodoma na Buswelu Mwanza, ambapo utekelezaji rasmi utaanza mwaka 2026/27.

Mbali na sekta ya makazi, Waziri huyo amesema NHC linaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya majengo ya biashara nchini, hatua inayochochea shughuli za kiuchumi pamoja na kuongeza thamani ya maeneo ya mijini.

Miradi hiyo ni pamoja na Meru View Shops Arusha iliyofikia asilimia 52, Tabora Commercial Complex asilimia 46, Singida 2F Plaza asilimia 85, Mkwakwani Commercial Complex Tanga asilimia 40, Kashozi Commercial Complex Kagera asilimia 65, Uluguru Plaza Morogoro asilimia 42 na Iringa Commercial Complex asilimia 40.

Aidha, Serikali imeeleza kuwa miradi ya biashara na ofisi katika maeneo ya Masasi, Mtanda Lindi na Zongomela Kahama imekamilika huku maandalizi ya mwisho ya miradi ya Usa River na Ngarenaro yakiendelea.

Katika eneo la ubia, Mhe. Dkt. Akwilapo amesema NHC linaendelea kusimamia miradi 21 ya ubia yenye thamani ya shilingi bilioni 351 ambapo miradi mitatu imekamilika na mingine ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji kwa wastani wa asilimia 56.

Amesema pia Shirika linaendelea kutwaa na kufufua miradi iliyokuwa imesimama kwa muda mrefu ili kuhakikisha uwekezaji huo unaleta tija kwa wananchi na Taifa kwa ujumla. Kati ya miradi 24 iliyokuwa imesimama, miradi 13 imekamilika huku mingine ikiendelea kushughulikiwa.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo amesema NHC limeendelea kuimarisha utendaji wake wa kifedha ambapo hadi Mei 15, 2026 limefanikiwa kupunguza madeni kutoka shilingi bilioni 27.98 mwaka 2024/25 hadi shilingi bilioni 19 mwaka 2025/26.

Pia, Shirika limeendelea na mpango wa ukarabati wa nyumba zake ambapo nyumba 1,283 kati ya nyumba 1,600 zilizopangwa kukarabatiwa tayari zimekamilika sawa na asilimia 80 ya lengo.

Kwa upande wa miradi ya ukandarasi na ushauri elekezi, Waziri Akwilapo amesema NHC limekamilisha ujenzi wa majengo nane ya Ofisi za Serikali katika Mji wa Serikali Mtumba Dodoma pamoja na jengo la Soko la Madini la Tanzanite Mirerani Manyara.

Kadhalika, ujenzi wa majengo ya TCRA Dodoma umefikia asilimia 73 huku mradi wa Zanzibar ukiwa umefikia asilimia 50.

Hotuba hiyo imeendelea kuonesha nafasi ya NHC kama chombo muhimu cha Serikali katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya makazi, biashara na huduma za ushauri elekezi nchini, huku Serikali ikiendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji na upatikanaji wa nyumba kwa Watanzania wa makundi mbalimbali.