NA DENIS MLOWE,IRINGA
MSAJILI wa Bodi ya Maziwa Tanzania Profesa George Msalya, ameendelea kutoa elimu kwa wananchi na wanafunzi kuhusu umuhimu wa kuongeza matumizi ya maziwa kama sehemu ya lishe bora nchini.
 Akiwahutubia wanafunzi wa Shule ya Msingi Sabasaba katika maadhimisho ya Wiki ya Maziwa Kitaifa yanayofanyika mkoani Iringa, Profesa Msalya alisema serikali imejipanga kuhakikisha kila Mtanzania, hususan watoto, anapata virutubisho muhimu kwa ukuaji wa mwili na akili.
Profesa Msalya aliwahakikishia wananchi kuwa timu ya Bodi ya Maziwa pamoja na viongozi kutoka serikali kuu, wataendelea kutembelea wafugaji nchini ili kuona huduma wanazotoa katika upatikanaji wa maziwa, pamoja na kujadili changamoto na fursa zilizopo katika sekta hiyo.
 Alisema kuwa kamati ya bunge ya viwanda, biashara, mifugo na kilimo itakuwepo Iringa kuona kazi inayofanywa na kutoa ushauri utakaosaidia kupanua wigo wa uzalishaji na matumizi ya maziwa.
Aidha, Profesa Msalya alisema kuwa Bodi ya Maziwa itaendelea kushirikiana na vyombo vya habari nchini ili kuhakikisha elimu ya matumizi ya maziwa inawafikia Watanzania kwa undani na kwa lugha nyepesi. Alibainisha kuwa elimu hiyo ni ya muhimu kwa kila mwaka, lakini katika Wiki ya Maziwa, hamasa hiyo imeongezwa ili kufikia makundi mengi zaidi.
Katika kuelekea kilele cha maadhimisho hayo, Profesa Msalya alisema kutafanyika kongamano kubwa la tano la wadau wa maziwa ambapo hoja na changamoto za tasnia hiyo zitajadiliwa kwa kina. Kongamano hilo litawakutanisha wazalishaji, wataalamu, wafanyabiashara, taasisi za serikali na wadau wengine muhimu.
Akizungumzia mikakati ya kuongeza hamasa ya unywaji wa maziwa nchini, Profesa Msalya alisema serikali imeanza kwa kuwekeza kwa watoto ambao ndio walaji wakuu na wanaohitaji zaidi virutubisho vinavyopatikana kwenye maziwa.
 Alieleza kuwa serikali ina mpango wa kudumu wa kuhakikisha maziwa yanapelekwa shuleni mara kwa mara, mpango ambao umeshaanza kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Serikali pia inaendelea kushirikisha walimu, wazazi, kamati za shule na wadau wa elimu ili kuhakikisha mpango huo unafanikiwa kwa asilimia kubwa, na kwamba watoto wanapata maziwa kama sehemu ya lishe yao ya kila siku.
Katika hatua nyingine, Profesa Msalya alitaja uwepo wa mradi mkubwa wa serikali wa mageuzi ya tasnia ya maziwa na mabadiliko ya tabia nchi. Kupitia mradi huo, serikali inakusudia kuanzisha vituo maalumu vya unywaji wa maziwa nchini kote vinavyojulikana kama baa za maziwa.
Amesema Vituo hivyo vitatoa maziwa peke yake, katika aina mbalimbali, kwa lengo la kuongeza upatikanaji wake kwa wananchi katika maeneo ya karibu.
Aidha, serikali inahamasisha unywaji wa maziwa maofisini, katika taasisi za serikali na sekta binafsi. Tayari baadhi ya ofisi zimeanza kutoa maziwa kwa watumishi wake kama sehemu ya kuhimiza afya bora na tija kazini. Profesa Msalya aliipongeza mifano hiyo na kuzitaka taasisi nyingine kuiga.
Kwa upande wa kuongeza uzalishaji, Profesa Msalya alisema kuwa serikali imejipanga kuhakikisha upatikanaji wa maziwa unaongezeka kutoka lita bilioni 2.2 za sasa hadi zaidi ya lita bilioni 13. Kupitia mradi wa mageuzi ya tasnia ya maziwa, serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 500 kwa ajili ya kuboresha miundombinu, barabara, ubora wa mifugo na maeneo mengine muhimu ili kuimarisha uzalishaji.
Alisisitiza kuwa ongezeko hilo litasaidia kuhakikisha Watanzania wanapata maziwa ya kutosha, afya za wananchi zinaimarika, uwezo wa kufikiri unaongezeka, na watoto wanapata virutubisho vinavyohitajika kwa ukuaji bora.