Tabora
Timu ya wataalamu kutoka Makao Makuu ya Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) kutoka Roma, Italia pamoja na Harare, Zimbabwe, imevutiwa na vivutio vya utalii vilivyopo mkoani Tabora baada ya kutembelea maeneo mbalimbali ya kihistoria na hifadhi za asili zilizopo chini ya usimamizi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Wataalamu hao wanne waliwasili mkoani Tabora Mei 24, 2026 kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Miombo katika Nyanda Kame za Magharibi mwa Tanzania (Integrated Landscape Management of Dry Miombo Woodland in the Western Parts of Tanzania), unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na FAO.
Baada ya shughuli za kikazi, ujumbe huo ulipata fursa ya kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo katika Ofisi ya Uhifadhi wa Misitu ya Asili Kanda ya Magharibi (DFC Tabora), ikiwemo Hifadhi ya Msitu wa Bwawa la Igombe pamoja na eneo la kihistoria la Tembe la Kwihara.
Wageni hao walieleza kufurahishwa kwao na namna safari hiyo ilivyoandaliwa kwa ustadi mkubwa, wakisifia mchanganyiko wa burudani, elimu na utalii wa asili uliowawezesha kujifunza zaidi kuhusu utajiri wa mazingira na historia ya Tanzania wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya kikazi.
Aidha, walieleza kuwa uzoefu walioupata katika kanda ya Magharibi umeonesha namna miradi ya uhifadhi wa mazingira inavyoweza kwenda sambamba na kukuza utalii endelevu na kuongeza thamani ya rasilimali za misitu nchini.

