📍Mwanza

Wakaguzi wa Migodi na Baruti nchini wametakiwa kuendelea kuzingatia sheria, kanuni na uadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuimarisha usimamizi wa shughuli za uchimbaji madini na kuongeza mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa taifa.

Wito huo umetolewa wakati wa kufungwa kwa Mkutano Mkuu wa Wakaguzi wa Migodi, ambapo Makamu Mwenyekiti wa Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, Fatuma Kyando amesema wakaguzi wanapaswa kutoa elimu kwa wachimbaji kuhusu sheria za madini ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya usimamizi wa sekta hiyo.

Amesema sheria zilizopo zinalenga kusaidia wachimbaji na hivyo ni wajibu wa wakaguzi kuhakikisha wachimbaji wanaelekezwa na kufahamu taratibu zote muhimu za shughuli za uchimbaji.

Kyando pia amesisitiza umuhimu wa kufanya vikao vya wakaguzi kwa vitendo zaidi kupitia ziara migodini, hususan migodi midogo yenye changamoto mbalimbali, ili kusaidia kutatua changamoto hizo kwa wakati.

Aidha, amewataka wakaguzi kuandika taarifa na kumbukumbu za ukaguzi wanazofanya migodini ili kuwa na rejea muhimu kwa ajili ya tathmini na maamuzi ya baadaye.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, Eng. Hamisi Kamando, amesema mkaguzi anatakiwa kuwa na uwezo mkubwa wa kitaaluma ili kusimamia kwa ufanisi shughuli za uchimbaji madini na kuhakikisha migodi inazingatia mifumo ya uchunguzi wa ajali kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizowekwa.

Amesema kuna umuhimu wa wakaguzi kuendelea kujijengea uwezo na kushirikishana uzoefu ili kuongeza ubora wa usimamizi wa sekta ya madini nchini.

Akirejea maelekezo ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Eng. Ramadhani Lwamo, Eng. Kamando amesema wakaguzi wanapaswa kutumia mbinu mpya za ukaguzi sambamba na kuzingatia uadilifu katika utendaji wao wa kazi.

Naye Meneja wa Baruti, Theresia Ntuke, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa usambazaji na matumizi ya baruti pamoja na kuongeza ushirikiano katika maeneo ya mipakani ili kudhibiti utoaji wa vibali vya kuingiza baruti nchini.

Kwa upande wake, Meneja wa Mazingira, Eng. Ephraim Mushi, amesema wakaguzi wanapaswa kushirikiana kwa karibu na wataalam wa mazingira na kutoa elimu kuhusu ufungwaji wa migodi katika vikao vyao ili kuimarisha usimamizi endelevu wa mazingira baada ya uchimbaji kumalizika.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki, Mhandisi Migodi Eng. Siri Boga amesema kongamano hilo limewapa fursa wakaguzi kujifunza, kubadilishana uzoefu na kuongeza uwezo wao wa kusimamia sekta ya madini kwa ufanisi zaidi.