📍 Bungeni,DodomaÂ
Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) imeendelea kuimarisha sekta ya viwanda nchini kwa kufanya tathmini ya viwanda, kuboresha maabara za kisasa pamoja na kuendeleza teknolojia za uzalishaji zinazolenga kuongeza thamani ya rasilimali za ndani.
Akizungumza leo Mei 22, 2026 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga amesema TIRDO imeendelea kutekeleza zoezi la tathmini ya viwanda na kubaini fursa za uwekezaji katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema tathmini hiyo inalenga kubaini idadi ya viwanda, ajira, uwezo wa uzalishaji, teknolojia zinazotumika pamoja na maeneo yenye fursa za uwekezaji ili kuchochea maendeleo ya viwanda na kuongeza thamani ya rasilimali za ndani.
Kwa mujibu wa Kapinga, zoezi hilo limefanyika katika mikoa miwili mipya na kufanya jumla ya mikoa iliyofikiwa kufikia tisa ambayo ni Pwani, Morogoro, Dar es Salaam, Kilimanjaro, Tanga, Arusha, Manyara, Mwanza na Shinyanga.
Aidha, amesema taarifa zote zilizokusanywa zimeingizwa katika mfumo wa kanzidata za viwanda ambapo hadi Aprili 2026 kulikuwa na jumla ya viwanda 25,650 vilivyosajiliwa.
“Kati ya viwanda hivyo, 482 ni vikubwa, 625 vya kati, 8,980 vidogo na 15,563 ni viwanda vidogo sana,” amesema Kapinga.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo amesema TIRDO imeendelea kuimarisha maabara zake kwa ajili ya utoaji wa huduma za kitafiti katika maendeleo ya viwanda.
Ameeleza kuwa maabara ya chakula iliyopata ithibati mwaka 2025 imeboreshwa kwa kuongeza huduma kutoka tatu hadi sita pamoja na kuongeza wigo wa bidhaa kutoka moja hadi nne.
Bidhaa hizo ni pamoja na vyakula vilivyotayari kwa matumizi, nyama na bidhaa zake, samaki na bidhaa zake pamoja na sampuli za usufi wa nyuso.
