Serikali imetoka rai Kwa wananchi kushiriki kutoa maoni juu ya maboresho ya Sheria ya Elimu, Sura ya 353 kupitia tovuti, Mitandao ya Kijamiiya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na mitandao mingine ya kijamii.

Akizungumza Mei 22, 2026, wakati wa kuhitimisha kikao cha siku mbili cha kupokea maoni ya wadau jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo amesema mchakato huo unalenga kupata maoni yatakayosaidia kuboresha sheria mpya ya elimu ili iendane na mahitaji ya sasa katika kuboresha sekta ya elimu.

Prof. Nombo amesema kila mwananchi ana nafasi ya kutoa maoni hadi mwezi Juni mwaka huu, ambapo baada ya hapo nyaraka mbalimbali zitaandaliwa kabla ya hatua inayofuata ya kuboresha ripoti na kukamilisha mchakato huo kwa ajili ya kuwasilishwa katika ngazi za maamuzi, ikiwemo Bunge.

Wakili na mjumbe kutoka Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), amesema matarajio yao ni kuona sheria mpya ya elimu inazingatia zaidi fursa za elimu jumuishi kwa watu wenye ulemavu.

Amesema ameridhishwa na namna ya ukusanyaji wa maoni ya sheria ilivyoweka bayana haki ya kundi hilo kupata elimu inayokidhi mahitaji yao, kwa kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayeachwa nyuma.

Naye, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Anna Ngalawa amesema mchakato wa ukusanyaji wa maoni ulikuwa shirikishi na wenye kutoa nafasi kwa wadau mbalimbali kushiriki.

Amesema matarajio yao ni kuona sheria mpya inatambua rasmi matumizi ya lugha ya alama katika ngazi zote za elimu na kuhakikisha lugha hiyo inakuwa somo rasmi la kufundishia shuleni.