Na Silivia Amandius.
Ngara , Kagera.
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeanza kufunga transforma mpya yenye uwezo wa megavoltiamperi tano (5MVA) katika Wilaya ya Ngara mkoani Kagera ikiwa ni jitihada za Serikali kuboresha huduma ya umeme na kuondoa changamoto ya kukatika kwa umeme kwa wananchi.
Hatua hiyo inatekelezwa kufuatia maelekezo yaliyotolewa na Waziri wa Nishati, Deogratias Ndejembi May 9 mwaka huu baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi wa Ngara kuhusu huduma ya umeme kutokuwa ya uhakika katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
Transfoma hiyo mpya imewasili katika kituo cha kupokea umeme cha Djululigwa ambapo wataalamu wa TANESCO wameanza kazi ya kuifunga, huku wakieleza kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika ndani ya saa chache ili kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Meneja wa TANESCO Wilaya ya Ngara, Mhandisi Amani Chidundo, amesema changamoto ya kukatika kwa umeme ilisababishwa na transforma ya zamani yenye uwezo wa 3MVA kushindwa kuhimili ongezeko kubwa la matumizi ya umeme kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi na kijamii wilayani humo.
Kwa upande wake, Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Ngara, Mkubila, amepongeza juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Nishati kwa kupeleka transforma hiyo mpya, akisema hatua hiyo italeta matumaini mapya kwa wananchi wa Ngara kwa kupata huduma ya umeme yenye uhakika na kusaidia kukuza maendeleo ya kiuchumi katika wilaya hiyo.

