Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega amesema ataendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi na uadilifu ili kuhakikisha malengo ya Serikali yanafikiwa kupitia mipango na miongozo mbalimbali ikiwemo Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025-2030.
Mhe. Ulega ameyasema hayo leo Jumatano, Mei 20, 2026, wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni jijini Dodoma.
Katika hotuba yake, Waziri Ulega ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kumuamini na kumteua tena kuwa Waziri wa Ujenzi kwa kipindi kingine.
“Niitumie nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuendelea kuniamini na kuniteua kuwa Waziri wa Ujenzi kwa kipindi kingine tena. Naomba kumuahidi Mheshimiwa Rais kuwa nitatekeleza majukumu haya kwa weledi na uadilifu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa kupitia miongozo na mipango mbalimbali ikiwemo Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2025,” alisema Waziri Ulega.
Aidha, amewahakikishia wananchi kuwa Wizara ya Ujenzi itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya miundombinu nchini kwa lengo la kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
