Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesisitiza kuunga mkono kikamilifu maazimio yote ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) na jitihada za kimataifa zinazolenga kuleta amani ya kudumu katika ukanda wa Mashariki ya Kati kupitia njia za kidiplomasia.
Msimamo huo umetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Ngwaru Maghembe (Mb), wakati wa maadhimisho ya miaka 78 ya Siku ya Nakba ya Taifa la Palestina yaliyofanyika Mei 16, 2026 jijini Dar es Salaam.
Akizungumza mbele ya wajumbe wa mashirika ya kidiplomasia na viongozi mbalimbali wa kiserikali, Dkt. Maghembe alieleza kuwa msimamo wa Tanzania katika suala la Palestina na Israel unajengwa juu ya misingi thabiti ya Sera ya Kutofungamana na Upande Wowote (Non-Alignment Policy).
“Katika muktadha huu, Tanzania inaendelea kuunga mkono maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na juhudi nyingine za jumuiya ya kimataifa zinazolenga kuendeleza mazungumzo ya kidiplomasia na utekelezaji wa mikataba mbalimbali inayolenga kutafuta amani kati ya Palestina na Israel.” Mhe. Maghembe alieleza.
Alibainisha kuwa utatuzi pekee wa kidiplomasia wenye tija ni ule unaozingatia suluhisho la “Mataifa Mawili” (Two-State Solution), ambapo Dola Huru ya Palestina itaishi bega kwa bega kwa amani na usalama kamili pamoja na Dola ya Israel. Aliongeza kuwa kupitia uongozi thabiti wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Tanzania itaendelea kuwa mstari wa mbele katika juhudi za kimataifa za kushawishi utekelezaji wa maazimio hayo, ili kuimarisha haki, ulinzi na usalama wa binadamu duniani kote.
Siku ya Nakba huadhimishwa kila mwaka tarehe Mei 15, kukumbuka zaidi ya wapalestina 750,000 waliopoteza makazi, ardhi na maisha yao, wakati wa vita vya mwaka 1948 kati ya Wapalestina na Waisraeli.

