Na Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Bungeni Dodoma 

Wizara ya Maliasili na Utalii imeomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi bilioni 334.3 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 ili kutekeleza malengo na vipaumbele mbalimbali vya sekta hiyo vinavyolenga kuimarisha uhifadhi, kukuza utalii na kuongeza mchango wa sekta katika uchumi wa Taifa.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo Bungeni mjini Dodoma, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji ameliomba Bunge kuidhinisha kiasi cha Shilingi 334,345,870,000 kwa matumizi ya Fungu 69 katika mwaka wa fedha 2026/2027.

Dkt. Kijaji amesema kati ya fedha hizo, Shilingi 272,044,425,000 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida huku Shilingi 62,301,445,000 zikielekezwa kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Amefafanua kuwa fedha za matumizi ya kawaida zinajumuisha Shilingi 144,691,490,000 kwa ajili ya mishahara ya watumishi pamoja na Shilingi 127,352,935,000 kwa matumizi mengineyo ya Wizara na taasisi zake.

Kwa upande wa miradi ya maendeleo, Waziri huyo alisema Shilingi 23,134,770,000 ni fedha za ndani huku Shilingi 39,166,675,000 zikiwa ni fedha kutoka vyanzo vya nje kwa ajili ya kuendeleza miradi mbalimbali ya kimkakati katika sekta ya maliasili na utalii.

Amesema fedha hizo zitasaidia utekelezaji wa vipaumbele vya Wizara ikiwemo kuimarisha uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori na misitu, kuboresha miundombinu ya utalii, kuimarisha matumizi ya teknolojia za kisasa pamoja na kuongeza nguvu katika utangazaji wa vivutio vya utalii ndani na nje ya nchi.

Ashatu Kijaji ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuona sekta ya utalii na maliasili kama nguzo muhimu ya uchumi wa Taifa kutokana na mchango wake katika ajira, mapato ya fedha za kigeni na maendeleo ya wananchi wanaozunguka maeneo ya hifadhi na vivutio vya utalii.