Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog,Bungeni Dodoma
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuwa Serikali imeendelea kupata mafanikio makubwa katika Sekta ya Maliasili na Utalii ambapo idadi ya watalii imeongezeka kufikia 5,935,561 mwaka 2025, ikiwa ni ongezeko la asilimia 10.7 ikilinganishwa na mwaka 2024.
Amesema kuwa ongezeko hilo linajumuisha watalii wa kimataifa na wa ndani, ambapo watalii wa kimataifa wameongezeka hadi 2,294,495 huku wa ndani wakifikia 3,641,066, hatua inayoonesha uimara wa sekta hiyo katika kuchangia uchumi wa taifa.
Ameyabainisha hayo Mei 15, 2026, Bungeni Jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2026/2027,
Amebainisha kuwa Tanzania imeendelea kuimarika kimataifa ambapo imeshika nafasi ya 11 duniani kwa ongezeko la wageni wa kimataifa ukilinganisha na kabla ya UVIKO-19, pamoja na kushika nafasi ya 6 barani Afrika na Mashariki ya Kati katika ukuaji wa wageni wa kimataifa.
Ameongeza kuwa mapato yatokanayo na utalii yameongezeka hadi Dola za Marekani bilioni 4.4 mwaka 2025 kutoka bilioni 3.9 mwaka 2024, hali iliyoifanya sekta hiyo kuwa ya pili kwa kuingiza fedha za kigeni nchini baada ya madini.
Aidha, amesema kuwa mafanikio hayo yametokana na maboresho ya miundombinu ya utalii, kuongezeka kwa utangazaji wa vivutio, pamoja na matumizi ya mifumo ya kidijitali katika kusimamia huduma na ukusanyaji wa mapato.
Katika hatua nyingine, ameongeza kuwa Serikali inaendelea kujiandaa na matukio makubwa ya kimataifa ikiwemo Mkutano wa IPU 2026, World Travel Awards 2026, Miss World 2027 na AFCON 2027, ambayo yanatarajiwa kuongeza zaidi idadi ya watalii na kukuza uchumi wa nchi.
Aidha, amesema kuwa Serikali itaendelea kuimarisha sekta hiyo kupitia mikakati ya kuongeza vivutio, kuboresha huduma za utalii na kuendeleza matumizi ya teknolojia ya kisasa ili kuongeza ushindani wa Tanzania kimataifa.
