Na Abduly Madenge, WAF – MOROGORO:
Serikali imewahakikishia wananchi kuwa kifo kutokana na kuchelewa kupata huduma za dharura sasa kinakwenda kubaki kuwa historia, kufuatia mkakati kabambe wa kusogeza huduma za kibingwa za uokoaji maisha karibu na makazi ya watu.
Kauli hiyo imetolewa Mei 14, 2026 mkoani Morogoro na Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Dharura na Maafa kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Erasto Sylvanus, wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha siku tatu kilicholenga kupitia miongozo ya matibabu ya wagonjwa mahututi (ICU) na mafunzo kwa vitendo kwa wataalamu wa afya.
Huduma za Dharura Mlangoni kwa Mwananchi Dkt. Sylvanus amebainisha kuwa tija ya maboresho haya kwa mwananchi ni kupatikana kwa huduma za dharura kwa haraka zaidi. Kupitia ushirikiano na TAMISEMI, jumla ya majengo ya kisasa ya dharura (EMD) 124 yamekamilika, ambapo 86 yapo kwenye ngazi ya msingi (halmashauri) na 38 kwenye hospitali za rufaa.
“Lengo la Rais wetu ni kuona mwananchi anapopata dharura kama ajali au mshtuko wa moyo, asisafiri umbali mrefu. Tumejenga majengo haya ili huduma ya kwanza ya kuokoa uhai ipatikane hapo hapo alipo,” alisema Dkt. Sylvanus.
Dkt. Erasto amesema Uimarishaji wa ICU na Vitengo vya Uangalizi Maalum umefanyika Katika kuhakikisha wagonjwa wanaohitaji uangalizi mkubwa wanapata huduma bora, Dkt. Sylvanus ameeleza kuwa serikali imefanya tathmini ya kina kwenye mikoa 13 na kuanzisha vitengo vipya vya uangalizi wa kati (HDTU) katika maeneo ya Kipawa, Buswelu, Mawenzi, Kasulu, na Temeke.
Hii inamaanisha kuwa wagonjwa mahututi sasa wanapata huduma bora bila kulazimika kwenda hospitali kubwa za mbali. Wataalamu Wenye Ujuzi na Moyo wa Kazi Ili majengo hayo yasiwe kuta tupu, Dkt. Sylvanus amesema Wizara imewekeza kwenye utaalamu kwa kufanya mambo yafuatayo
Dkt. Erasto ameongeza kuwa Maabara za Kisasa zimejengwa na Zimeanzishwa katika hospitali sita (KCMC, Muhimbili, MUHAS, BMH, Bugando, na MZRH) kwa ajili ya kufundisha watumishi namna ya kuokoa maisha kwa vitendo, sambamba na Mafunzo kwa Watumishi ambapo Zaidi ya wataalamu wa afya 1,728 kutoka mikoa 10 tayari wamejengewa uwezo na kupatiwa ushauri elekezi ili kutoa huduma kwa upendo na weledi.
Kuhusu Tija ya Kikao Kazi cha Morogoro
Dkt. Sylvanus amehitimisha kwa kusema kuwa kikao hicho cha Morogoro ni muhimu kwa mwananchi kwa sababu kinakwenda kuweka “ramani” moja ya jinsi ya kumtibu mgonjwa mahututi nchi nzima.
“Tunatengeneza miongozo ambayo itahakikisha mwananchi anayetibiwa ICU Morogoro, anapata ubora wa huduma ule ule angeupata Muhimbili au nje ya nchi. Huu ni uwekezaji mkubwa kwenye utu na uhai wa Mtanzania,” alisisitiza Dkt. Erasto.

