Na Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma

Jamii mkoani Dodoma imetakiwa kuendelea kujenga mazingira ya usawa na haki kwa wanawake, watoto wa kike pamoja na makundi maalum ili kuongeza ushiriki wao katika shughuli za maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Wito huo umetolewa Mei 14,2026 Jijini Dodoma wakati wa mjadala ulioandaliwa kupitia Mradi wa Tuinuke Pamoja unaotekelezwa na Aga Khan Foundation uliowakutanisha viongozi wa dini, wazee wa mila, maafisa maendeleo ya jamii pamoja na vikundi vya wanawake kutoka Wilaya za Bahi, Chamwino na Dodoma Jiji.

Mratibu wa Masuala ya Kijinsia wa taasisi hiyo kutoka Makao Makuu Dar es Salaam, Bi. Zaibu Mmari amesema kuwa mradi huo umejikita katika kutoa elimu ya usawa wa kijinsia na kuhamasisha jamii kushirikiana kuondoa changamoto zinazochochea ukosefu wa haki kwa wanawake na watoto wa kike.

Aidha, amebainisha kuwa kupitia mijadala hiyo wananchi wamekuwa wakipata nafasi ya kujadili mila, desturi na mifumo inayoweza kuathiri maendeleo ya wanawake pamoja na kutafuta njia bora za kujenga jamii yenye ushirikishwaji kwa wote.

Pia ameongeza kuwa mradi huo unaofadhiliwa na Embassy of Ireland Tanzania unatekelezwa kuanzia Julai 2024 hadi Juni 2027 kwa lengo la kufikia halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma na kusaidia kuwawezesha wanawake, vijana na makundi maalum katika nyanja za kijamii na kiuchumi.

Kwa upande wake, Afisa Mradi wa Tuinuke Pamoja Wilaya ya Bahi, Erick Maurid amesema kuwa mradi huo pia unatoa mafunzo ya biashara na ujasiriamali kwa vikundi mbalimbali ili kuongeza uwezo wa wananchi kujitegemea kiuchumi.

Aidha, amebainisha kuwa ushiriki wa viongozi wa dini na wazee wa mila katika mijadala hiyo unasaidia kufikisha ujumbe wa usawa wa kijinsia kwa jamii kwa urahisi zaidi kutokana na nafasi yao katika jamii.

Washiriki wa mjadala huo wameitaka jamii kuendelea kutoa malezi yanayozingatia usawa kwa watoto wa kike na wa kiume pamoja na kuboresha mifumo ya kijamii na kisheria ili kuhakikisha haki zinapatikana kwa makundi yote bila ubaguzi.