Katibu Tawala wa Wilaya ya Arusha, Jacob Rombo akizungumza kwenye hafla hiyo jijini Arusha leo

Happy Lazaro,Arusha .

Arusha .Katibu Tawala wa Wilaya ya Arusha, Jacob Rombo amewataka wanawake wajawazito kuacha tabia ya kujifungulia majumbani na badala yake kutumia vituo vya afya na hospitali kwa ajili ya huduma salama za uzazi.

“Serikali imewekeza fedha nyingi kuhakikisha kina mama wanajifungua salama katika vituo vya afya vyenye wataalamu na vifaa tiba vya kisasa. Tuachane na kujifungulia nyumbani au kwenda kwa waganga wa kienyeji,”amesema Rombo.

Rombo aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude ameyasema hayo leo jijini Arusha wakati akizungumza katika 

zoezi la upimaji wa magonjwa mbalimbali pamoja na utoaji wa matibabu bure kwa wakazi wa Jiji la Arusha kwa muda wa siku mbili unaoendelea katika hospitali ya Kaloleni jijini Arusha .

Aidha Rombo amewahimiza wananchi kutumia huduma zinazotolewa hospitalini hapo, kuzingatia usafi wa mazingira pamoja na kujiunga na mifumo ya bima ya afya ili kurahisisha upatikanaji wa matibabu.

Aidha amewataka watumishi wa afya,kuendelea kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na moyo wa huruma kwa wananchi, akisisitiza kuwa afya bora ni msingi wa maendeleo ya taifa.

Rombo amesema kuwa, amesema mafanikio ya hospitali hiyo yatategemea ushirikiano wa wananchi wote katika kuitunza, kuilinda na kuhakikisha vifaa pamoja na huduma zilizowekwa zinawanufaisha wananchi kama ilivyokusudiwa.

Amesema hospitali hiyo ni mali ya umma iliyojengwa kwa fedha za walipa kodi, hivyo kila mwananchi ana wajibu wa kuhakikisha mali zote zilizopo zinatunzwa na kulindwa dhidi ya ubadhirifu.

“Tusione jukumu la kuitunza ni la walinzi au viongozi pekee. Kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha vifaa, dawa na mazingira ya hospitali vinabaki salama kwa manufaa ya jamii,” amesema Rombo.

Amewataka wananchi kutoa taarifa kwa viongozi au uongozi wa hospitali wanapoona vitendo vya wizi, uharibifu wa vifaa tiba au matumizi mabaya ya mali za umma.

“Serikali ya Samia Suluhu Hassan itaendelea kuboresha sekta ya afya kwa kusogeza huduma muhimu karibu na wananchi pamoja na kuongeza uwekezaji katika vifaa tiba na rasilimali watu.”

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Shaban Manyama, amesema Halmashauri ya Jiji la Arusha imeweka mkakati wa kuwa na hospitali tatu za wilaya kwa lengo la kusogeza huduma bora za afya karibu zaidi na wananchi.

Manyama amesema kwa sasa tayari jiji hilo lina hospitali mbili za wilaya ambazo ni Hospitali ya Wilaya ya Njiro pamoja na Hospitali ya Wilaya ya Kaloleni iliyozinduliwa rasmi, huku juhudi zikiendelea kuhakikisha hospitali hizo zinaimarishwa kwa vifaa tiba vya kisasa pamoja na wataalamu wa afya wa kutosha.

“Tunalenga kuhakikisha wananchi wa Arusha hawalazimiki kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya. Ndiyo maana tunaendelea kuboresha miundombinu ya hospitali, kuongeza vifaa tiba pamoja na watumishi wa afya ili huduma ziwe bora zaidi,” amesema Manyama.

Aidha, amesema kupandishwa hadhi kwa Kituo cha Afya Kaloleni kuwa Hospitali ya Wilaya ni hatua kubwa katika kuimarisha huduma za afya jijini humo, kwani itaongeza uwezo wa kutoa huduma mbalimbali za kibingwa ambazo hapo awali zilikuwa zinapatikana katika hospitali kubwa pekee.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arusha, Willfred Soilel, aliutaka uongozi wa hospitali zote jijini humo kuhakikisha unatanguliza utoaji wa huduma kwa wagonjwa badala ya kuweka mbele malipo, ili kuokoa maisha ya wananchi na kupunguza vifo vinavyoweza kuepukika.

Soilel amesema baadhi ya wananchi wamekuwa wakikumbana na changamoto ya kucheleweshewa huduma kutokana na taratibu za malipo, hali ambayo wakati mwingine huweka maisha ya wagonjwa katika hatari.

“Huduma kwa mgonjwa inapaswa kuwa kipaumbele cha kwanza. Tusikimbilie malipo kabla ya kuokoa maisha ya watu. Wananchi wanapofika hospitalini wanahitaji kupewa huduma kwa wakati ili kuepusha madhara makubwa zaidi,” amesema Soilel.

Hafla hiyo iliambatana na maandamano ya watumishi wa jiji na wauguzi kutoka ofisi ya Mkuu wa wilaya hadi katika hospitali hiyo na zoezi maalumu la upimaji wa magonjwa mbalimbali pamoja na utoaji wa matibabu bure kwa wakazi wa Jiji la Arusha, ambapo wananchi wengi walijitokeza kupata huduma hizo.