Na John Walter -Babati

Samia Suluhu Hassan ametajwa kuwa ni kiongozi mchapakazi anayejali maslahi ya wananchi kutokana na jitihada zake za kuwaletea maendeleo Watanzania katika sekta mbalimbali.

Kauli hiyo imetolewa na Catherine Canute Joachim wakati akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Wazazi kimkoa yaliyofanyika katika kata ya Ufana wilayani Babati Vijijini mkoani Manyara.

Dkt. Catherine amesema serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kugusa maisha ya wananchi kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta za afya, elimu, maji na miundombinu.

Aidha amesema Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kuwatumikia wananchi na kuhakikisha maendeleo yanaendelea kufika kwa wananchi wa maeneo mbalimbali nchini.

Maadhimisho hayo ya Wiki ya Wazazi yalifanyika chini ya kauli mbiu isemayo, “Malezi bora na uzalendo ni msingi wa taifa.”

Katika maadhimisho hayo, shughuli mbalimbali za kijamii zilifanyika ikiwemo upandaji miti katika Kituo cha Afya Ufana pamoja na ugawaji wa taulo za kike kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Ndeki ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono afya na ustawi wa mtoto wa kike.